TASWIRA ZA MGOMO WA MADEREVA MWANZA






Mabasi yanayoenda mikoani yakiwa yamepaki katika Kituo cha Mabasi cha Nyegezi mkoani Mwanza kufuatia mgomo wa Umoja wa Vyama vya Madereva nchini wakishinikiza serikali kutatua kero zinazowakumba madereva hao.
Maofisa polisi wa Jiji la Mwanza wakijadiliana jambo katika Kituo cha Mabasi cha Nyegezi wakati wa mgomo huo.




Abiria wakiwa wamesimama ndani ya eneo la Kituo cha Mabasi cha Nyegezi baada ya kukoswa usafiri kufuatia mgomo huo, huku askari polisi akihakikisha ulinzi na usalama katika eneo hilo.
Abiria na wakazi wengine wa Jiji la Mwanza wakitaharuki mgomo wa madereva hapo Nyegezi.
Baadhi ya wasafiri wakizungumza na maofisa polisi wa Mkoa wa Mwanza katika Kituo cha Mabasi cha Nyegezi.
Baadhi ya abiria waliokwama kusafiri wakiwa kwenye makundi wakijadili hatima yao.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga (kushoto) akiongozana na Ofisa wa polisi mkoani Mwanza kukagua kituo cha Mabasi cha Nyegezi.
Mkuu wa Wilaya akiwatangazazia abiria waliokwama kuondoka waingie kwenye magari ili waanze safari zao, lakini abiria walipoingia hakuna gari lililoondoka kituoni hapo.
Mkuu wa Wilaya akizungumza na Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Mkoa wa Mwanza Bw. Shaban Wandiba.
Na Johnson James, GPL- Mwanza
MADEREVA wanaoendesha mabasi ya abiria waendao mikoani wamegoma kuendesha magari yote yanayofanya safari zake kutoka jijini hapa kuelekea maeneo mbalimbali hapa nchini kutokana na baadhi ya viongozi wao ambao wako jijini Dar es Salaam kukamatwa na polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Mkoa wa Mwanza, Shaban Wandiba amesema kuwa “sisi kama Umoja wa Madereva wa Mabasi yaendayo mikoani, tumepokea taarifa kuwa kuna baadhi ya viongozi wetu walioko huko Dar es Salaam wamekamatwa wakati wao ndio watetezi wetu hivyo baada ya madereva kusikia hivyo wakasema kuwa hawataondoa magari mpaka viongozi hao waachiwe huru na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.”
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana jijini hapa, Baraka Konisaga amesema kuwa hakuna haja ya wananchi kuendelea kuteseka katika maeneo ya kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Nyegezi bila sababu za msingi kama kuna baadhi ya magari yameamua kugoma yapishe njia ili wanaotaka kuwasafirisha abiria waendelee na safari zao.
Hata hivyo licha ya mkuu huyo wa wilaya kutoa tamko kwa wamililiki wa mabasi ya Bunda, Happy Nation, Zuberi na mengine kuwa waondoe magari yao mgomo huo umeendelea na hakuna dereva hata mmoja aliyejitokeza kuwasha gari kuashiria kuanza safari ya kusafirisha watu.



Aidha nao baadhi ya abiria waliofika mapema katika Kituo cha Mabasi cha Nyegezi kwa ajili ya kusafiri na kukumbana na adha hiyo wamesema kuwa “Sisi hatukuwa na taarifa za mgomo huu na kama tungekuwa na taarifa yake tusinge kata tiketi kwa ajili ya safari hivyo wengine hapa tunaenda Dar kuangalia wagonjwa hivyo tunaiomba serikali iingilie kati mgomo huu, wazungumze na hawa madereva wajue nini tatizo na wajue jinsi gani ya kutatua matatizo haya yaliyopo".
Nao wamiliki wa magari hayo yaendayo mikoani wamesema kuwa hawautambui mgomo huo na watawaambia madereva wao kuwasafirisha abiria hao waliokata tiketi kwa jana ili wafike kwa wakati licha ya kuchelewa kuanza safari hata hivyo licha ya wamiliki wa magari kutoa kauli nzito kwa madereva wa magari yao madereva hao wamegoma kuondoa magari hali iliyofanya abiria waliofika katika kituo cha Nyegezi kuwa katika hali ya sintofahamu baada ya madereva hao kutoonekana katika maeneo hayo.
Mpaka mwandishi wa habari hii anatoka eneo la tukio hakuna gari hata moja ambalo lilikuwa limeondoka maeneo hayo.