Na Mwandishi Wetu
KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT- Tanzania, Zitto Kabwe ametaja sifa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye angependa aongoze nchi na kusema kwamba yeye ana sifa hizo.
KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT- Tanzania, Zitto Kabwe ametaja sifa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye angependa aongoze nchi na kusema kwamba yeye ana sifa hizo.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Zuberi Kabwe.
Akizungumza na kituo kimoja cha runinga mwishoni mwa wiki iliyopita, Zitto alisema mtu anayetaka kuwa rais wa nchi hii ni lazima awe na uzalendo na asiwe ‘kasuku’ wa maneno mengi bila kuwa na sifa ya kusogeza nchi mbele kimaendeleo.Alisema sifa nyingine ya anayefaa kuwa rais ni lazima mgombea nafasi hiyo achukie wananchi kuwa maskini kwa sababu nchi yetu ina fursa nyingi za kuwaondoa raia wake katika hali hiyo.
Aliongeza kuwa mgombea nafasi hiyo nyeti ya uongozi wa juu wa nchi ni lazima awe anayependa kuunganisha nchi na siyo kufarakanisha na awe wazi katika utawala wake akitolea mfano uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alisema ameweka wazi Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CIG).
“Rais Kikwete tayari ameweka misingi ya jambo hilo la ripoti ya CIG kama tulivyoona, hii inatakiwa kila wakati iwe wazi. Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa kwa miaka mitano ya mwisho aliyokaa madarakani hakutoa hadharani ripoti hiyo, jambo ambalo ni baya,” alisema Zitto.
Aliongeza kuwa wakati umefika kwa rais ajaye kuweka mfumo wa utawala mzuri na kupambana na ule unaowanufaisha wachache katika nchi yetu kutokana na ‘keki ya taifa.’
Alipoulizwa kama katika sifa hizo alizozisema kuna yeyote anaweza kumtaja kati ya waliojitokeza kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema hawezi kukisemea chama hicho kwa sababu kina taratibu zake na vigezo vyake vya kumpata mgombea wao japokuwa yeye anazo kwani ni mfuasi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa na itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea.
Zitto alihojiwa pia kama yeye atagombea urais alijibu kuwa umri haumruhusu, hata hivyo, alisema yeye amejiandaa kugombea ubunge katika jimbo jipya na siyo Kigoma Kaskazini.
Alipotakiwa atoe sababu za kutogombea Kigoma na badala yake anataka kugombea kwingine alisema: “Kigoma Kaskazini nimewatumikia wananchi wake kwa miaka kumi naamini nilichowafanyia kinatosha, nikawaaga. Nataka nimpishe mtu mwingine mimi nigombee kwingine kwani nimeshapata maombi katika majimbo kadhaa.
“Naweza kugombea Jimbo la Segerea, Ubungo, Kahama na Kawe kwa sababu wananchi wa majimbo hayo wanataka nikawatumikie lakini uamuzi wa wapi nitagombea, itategemea uamuzi wa vikao vya chama changu ambacho kitanipangia nikagombee wapi.”
Alitamba kwamba chama chake kipya ni kama moto wa pimba ambazo juu unaweza kudhani umezimika lakini ndani upo mkali sana.
Juzi Zitto amewaambia waandishi wa habari jijini Dar kuwa chama chake kina uhakika wa kuwa na wabunge 50 ambao watatoka vyama mbalimbali vikiwemo chama tawala, Chama Cha Mapinduzi, (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)na The National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR Mageuzi).
“Nahitaji majimbo yote ya Kigoma kuchukuliwa na ACT bila kukosa hata moja,” alisisitiza Zitto.
Kauli hiyo inawagusa moja kwa moja wabunge wa sasa wa majimbo ya Kigoma ambao ni Felix Mkosamali (Muhambwe),Moses Machali (Kasulu Mjini), Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) na David Kafulila (Kigoma Kaskazini) pamoja na Peter Serukamba (Kigoma Mjini), Christopher Chiza (Buyungu) na Albert Obama(Manyovu).