HIVI majuzi moja kati ya habari za burudani ambazo zilisikika zaidi katika vyombo vya habari ni kuhusiana na suala zima la mwanamuziki Ally Choki pamoja na dansa mahiri Super Nyamwela kurejea kwenye bendi ya Twanga Pepeta.
Wawili hao walikuwa moja kati ya wahasisi wa bendi hiyo ambapo waliisaidia kufahamika zaidi hasa pale ambayo ilikuwa imeanza kabla ya kuondoka na kuanzisha bendi ya Extra Bongo iliyokuwa ikiongozwa na Ally Choki.
Wawili hao wameamua kurejea tena kwenye bendi ya Twanga Pepeta baada ya ile bendi ya Extra Bongo kushindwa kusonga mbele tena kutokana na sababu mbalimbali.
Binafsi sitaki kuonesha ni kwa kiasi gani Choki amerudi nyuma kimaendeleo ya sanaa kwa kurejea kwake katika bendi yake ya zamani ila ninapenda kuzungumzia ni nini kifanyike kwa wanamuziki ambao wanaamua kuanzisha bendi zao ikli waweze kuendelea zaidi.
Ifahamike kuwa kwa mwanamuziki akianzisha bendi yake anakuwa amefungua milango ya ajira kwa wanamuziki wengine.
Anakuwa ameweka mazingira kwa wacheza dansi, wanamuziki, watumiaji wa vyombo vya muziki kujipatia ajira kwa hiyo uamuzi wa kuanzisha bendi unakuwa umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza wigo wa ajira kwa wasanii na kuendeleza sanaa nzima kwa ujumla.
Kilichotokea kwa Extra Bongo kushindwa kuendelea katika soko inamaana kuwa kuna watu wengi wameshakosa ajira hasa wale waliokuwa wameajiliwa na bendi hiyo.
Ili kuondokana na hali kama hiyo kujitokeza tena inatakiwa kwa wanamuziki wanapoamua kuanzisha bedni wazingatie yale ambayo yanatakiwa kufanyika ili kuhakikisha kuwa bendi hizo zinazidi kukua.
Ni vema wakahusisha wataalamu katika kuendesha biashara kama hizo kwa mfano kuwa na meneja mwenye ujuzi na uwezo wa kazi hiyo, kuwa na watu wa kuitangaza bendi na kuhakikisha kuwa inafanya vema sokoni.
Inatakiwa kwa wamiliki wa bendi pia kuhakikisha kuwa wanazingatia yale ya msingi katika kuendesha bendi kama vile kuwa na mtaji wa uhakika kuwa na nidhamu ya kazi pamoja kuwa na kazi nzuri za sanaa ili kujihakikishia maendeleo zaidi.
Kwa kufanya angalau mambo kama hayo itasaidia kuongeza ufanisi wa bendi zetu na kujikuta zikiendelea kudumu katika chati.
Kitu kikubwa kinachosababisha bendi zetu kushindwa kuhimili ushindani katika soko la sanaa ni kukosekana kwa watu wenye sifa stahiki katika kuendesha bendi hizo.
Bendi kama Yamoto inaweza kuendelea kuwa kwenye chati kwa muda mrefu kwa kuwa wamiliki wake ni watu ambao mbali na kuujua muziki lakini pia wanaweza kulisoma soko la muziki na kuona ni nini wafanye ili waendelee kuwa kwenye chati.
Kurejea kwa Ali Choku Twanga Pepeta kunatoa picha kuwa bado wanamuziki wetu wengi hawajaiva katika kumudu kuendesha bendi zao wenyewe au hata zile za kupewa kuendesha.
Wapo wanamuzi wengine walianzisha bendi zao nazo zikajikuta zikishindwa kufanya vema kama vile Muumini Mwijuma alianzisha Bendi ya Bwagamoyo, huku kukiwa na bendi kama Stono Mayasika na nyinginezo ambazo zilianzishwa na kuhasisiwa na wanamuziki na kwa sasa zimekufa.
Inatakiwa wanamuziki kujifunza mengi zaidi katika fani hiyo hasa suala zima la kuongoza bendi ili kujihakikishia kumudu ushindani na sio kushindwa.
Nimpongeze pia Asha Baraka kwa kuwa ameonesha kuwa kweli ni mlezi wa wasanii kwa kuwa wamekuwa wakipita kwake na kutoka kujaribu kuanzisha bendi nyinginezo zinazomletea ushindani na baada anawapokea tena.
Ningependa kumalizia kwa kuwashauri wanamuziki kuwa makini katika kuendesha biashara zao za bendi wanapoamua kuzianzisha na tena wanatakiwa kuomba ushauri kutoka kwa watu wenye uwezo wa kuongoza bendi.