MCHUNGAJI Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Gwandu Mwangasa, amesema kamwe hawawezi kuhamisha kanisa lao lililopo katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) kumnukuu Meneja Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Yahaya Charahani akisema wametoa notisi ya mwezi mmoja kwa kanisa hilo linaloongozwa na Mchungaji Josephat Gwajima kuhama katika viwanja hivyo.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mchungaji Mwangasa alisema taarifa hizo si kweli, kwani wao hawana mpango wowote kwa sasa kuondoka katika eneo hilo.
“Hizo ni taarifa tu za uongo, hazina ukweli wowote, ili upate ukweli kuhusu taarifa hizi mpigie Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba, Nehemia Mchechu ndiye atakayekupa taarifa zote, wengine watakudanganya,” alisema Mchungaji Mwangasa.
Naye Msemaji wa Askofu Gwajima, Yekonia Behanaze, alisema hawana taarifa zozote kutoka NHC zinazowataka kuhama katika eneo hilo kama ambavyo inasambazwa katika mitandao ya kijamii na kwenye baadhi ya magazeti.
“Ndugu mwandishi sina taarifa yoyote juu ya suala hilo, kwanza ndiyo nazisikia kutoka kwako, hivyo ngoja nianze kuzifanyia kazi ili nijue ukweli wa jambo hilo,” alisema Behanaze.
Taarifa ya NHC ilieleza kuwa Askofu Gwajima alipatiwa notisi ya kuhama katika eneo hilo la Kawe mwezi mmoja uliopita ingawa hakuitekeleza badala yake ameendelea kutumia eneo hilo kuendesha shughuli za kanisa lake, ikiwamo ibada.
Charahani alisema eneo hilo ni mali ya NHC na ni maalumu kwa ajili ya ujenzi wa mji wa kisasa na wakazi waliokuwa wakiishi katika eneo hilo tayari walikwishalipwa fidia zao muda mrefu.
Alisema hiyo si mara ya kwanza kwa NHC kumwandikia notisi Askofu Gwajima ambapo alisema notisi ya kwanza ilikwisha tangu Machi 9 mwaka huu na tangu wakati huo walimwongezea siku kadhaa ambazo zilikuwa zinamalizika jana.
Kwa wiki tatu sasa, Askofu Gwajima amekuwa gumzo katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii baada ya kuitwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa maneno ya kashfa hadharani dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Katika mfululizo huo, Gwajina alianguka na kuzimia wakati akihojiwa na polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na baadaye kulazwa Hospitali ya TMJ kabla ya kuruhusiwa na kutoka huku akitumia kiti cha magurudumu cha kubebea wagonjwa (wheelchair).
Askofu Gwajima baadaye aliibukia katika kanisa lake na kuongoza ibada katika Sikukuu ya Pasaka, akiwa katika kiti chake cha matairi na baadaye jioni aliweza kusimama na kutembea baada ya kuombewa na wachungaji kutoka nchini Japan ambao walikuja nchini kwa ajili ya kumjulia hali.