SEKTA ya
mavazi ni moja kati ya sekta za kiutamaduni ambazo zinazidi kukua kwa kasi huku
changamoto kubwa ikiwa ni kulipata vazi la taifa.
Sio suala geni kusikika masikioni mwa watu
wakizungumzia upatikanaji wa vazi hilo la taifa kwa kwa kumekuwa na michakato
mbalimbali iliyokwishawahi kufanywa na wadau mbalimbali katika kulipata vazi
hilo.
Lakini pia katika kuendeleza utamaduni huo wa
upatikanaji wa vazi hilo kumekuwa na maonesho mbalimbali ya mavazi ambayo
yamekuwa yakifanyika sambamba na kuendeleza utamaduni wa mavazi chini.
Maonesho kama Lady in Red, Swahili Fashion, Usiku
wa Kanga za Kale, Malaika na mengineo yotee yanalenga kukuza utamaduni huo wa
mavazi.
Ili kuendeleza utamaduni huo kuna wabunifu
mbalimbali ambao kila kukicha wamekuwa wakibuni mavazi kulingana na uhitaji wa
soko kwa wakati husika.
Mbunifu Evelyn Rugemalila wa Eve Collection
anasema kuwa kwa sasa soko kubwa lipo kwenye nguo za maharusi pamoja na sherehe
za Kitchen Party mahsus kwa akina mama.
Anasema kuwa kwa upande wake anaona kuwa fursa
katika soko hilo ndio inatoa mwanya wa ajira kwa watu wengi kwa sasa wanaojishughulisha
na kazi za ubunifu.
Anasema kuwa wanadada wengi kwa sasa wanatambua
kazi za wabunifu wa ndani na wamekuwa wakiwatumia katika kuwashone nguo zao za
kibunifu.
Anaongeza kuwa kwa upande wake amekuwa akipata
fursa za kuwashonea wanawake wengi hasa katika hafla mbalimbali.
“Inatakiwa kuwepo kabisa na sera kwanza ya
kulinga hakimiliki ya kazi ya mbunifu wa mavazi hasa katika kutambua kazi zao,
lakini pia inatakiwa kwa wabunifu pia kuzidisha ubunifu wa kazi ili kuendeleza
tasnia hii inayokua kwa kasi hapa nchini”anasema Evelyn.
Ili kuendelea kuwa na wabunifu wakubwa wa mavazi
hapa kama akina Mustapha Hasanali, Evelyn Rugemalila na wengineo inatakiwa pia
kuwepo na mikakati endelevu ya kuwavumbua na kuwaendeleza wabunifu chipukizi
hapa nchini.
Wapo wabunifu ambao mbali na kuwa na vipaji
lakini havijaonekana na kufanyiwa kazi ipaswavyo na kuwawezeesha kuchangia
kikamilifu maendeleo ya tasnia hiyo.
Mratibu Wiki ya Mavazi ya Swahili Fashion, Honest
Arroyal anasema kuwa kupitia wameanzisha shindano la la kuvumbua vipaji
lijulikanalo kama Emerging Designer Awards.
Anaongeza kuwa ni katika shindano hilo ambapo
wabunifu chipukizi wanaonesha uwezo wao katika ubunifu wa mavazi na kasha
anachaguliwa mbunifu mmoja ambae ndio anatangazwa kuwa ni mshindi.
Anasema kuwa chini ya utaratibu kama huo wabunifu
kama akina, Martin Kadinda, Pooja Jeshang, Sara Mosengo Aly Salim wa Mkoto
Design na wengineo wamepatikana.
Anafafanua kuwa kwa mwaka huu ambapo onesho hilo
litafanyika Desemba 6, 7 na 8 pia kutakuwa
na shindano kwa ajili ya wabunifu chipukizi.
Anaongeza kuwa hadi sasa wabunifu wengi
wameshajitokeza na kuchukua fomu za ushiriki ikilinganiwa na miaka ya nyuma.
“Najua ili kukuza utamaduni huu wa mavazi na
kuipa tasnia hii heshima inayostahili inatakiwa kuwepo kwa mikakati ya kisasa
kabisa ya kuwaibua wabunifu na Swahili Fashion ndipo mahala pake”anasema
Arroyal.
Kwa upande wake Martin Kadinda anasema kuwa
kupitia maonesho ya mavazi ndipo vipaji vingi vinaibuliwa na kuwatengenezea
mwanya wa ajira vijana.
Anaongeza kuwa anaona kuwa kwa sasa hata wasanii
wamekuwa wakivalia nguo za wabunifu wa mavazi wa hapa hapa nyumbani.
Anaongeza kuwa kwa kufanya hivyo inaonesha ni kwa
kiasi gani tasnia hiyo ya ubunifu wa mavazi inahusiana na sanaa ya muziki kwa
ukaribu zaidi.
“Kwa mimi binasfi nilikua nikimvalisha msanii
Nasib Abdul, Diamond kwa kipindi kirefum, na amekuwa akionekana nadhifu tena
vema sana, hiyo ni kwa kazi yangu mimi kama mbunifu wa mavazi”anasema Kadinda.
Anaongeza kuwa kwa wasanii wa Marekani na
kwengineko duniani hali imekuwa ni tofauti kwa kuwa wao wenyewe wanauza nguo
zao na wanapata mabilioni ya fedha.
Hilo linajidhihirisha kwa msanii mahiri
wa Marekani ambae leo anatumbuiza kwenye Tamasha la Serengeti
Fiesta mwaka T.I.
Msanii huyo anamiliki mavazi yenye lebo
mbalimbali kama vile Hustle Gang, Akoo pamoja na Strivers Row ambayo yameanza
kuuzwa kwenye duka la Pop Up Shop lililopo Super Market ya Dar Free Market.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Grand Hustle
Records, Jason Geter ambayo ndio kampuni inayomsimamia msanii B.O.B na
mwanadada anayekuja kwa kasi Iggy Azalea wa Marekani, anasema
anaamini soko la Tanzania na Afrika kwa ujumla ni masoko makubwa kwa bidhaa zao.
‘Tuna
matarajio makubwa kuhusiana na kuleta bidhaa zetu nchini Tanzania, na tunatarajia
sio tu kuleta bidhaa zetu hapa nchini, bali kwenda mbali zaidi kwa kujifunza
soko la mitindo hapa nchini’ anasema Geter.
Anaongeza
kuwa wasanii wanatakiwa kutumia umaarufu wao katika kujitafutia vyanzo vingine
vya biashara muhimu.
a