Kabla ya kwenda kucheza soka la kimataifa Vietnam na Oman Mrwanda alikuwa amewahi kuzichezea klabu za AFC ya Arusha na Wekundu wa Msimbazi Simba
KLABU ya Yanga imefanikiwa kupata saini ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Dan Mrwanda aliyekuwa akiichezea Moro United kwa mkopo wa muda mfupi akitokea timu ya Don Long Tan ya Vietnam.
Mshambuliaji huyo aliyeifungia Polisi Moro mabao manne kwenye mechi saba alizoichezea timu hiyo alisema amesaini mkataba wa mwaka mmoja ambao utamweka hadi mwanzoni mwa msimu wa 2015/2016 huku mkataba huo ukiwa makubaliano ya kuongezwa muda endapo mchezaji huyo ataonyesha kiwango cha juu.
Kabla ya kutua Jangwani Mrwanda alikuwa akifukuziwa kwa karibu na klabu za Simba na Azam lakini zilichelewa kufanikisha mpango huo hadi hapo viongozi wa Yanga walipoingilia kati na kunasa saini ya mkongwe huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupachika mabao.
Kocha wa Yanga Mbrazili Marcio Maximo ameiambia Goal kuwa wamemsajili Mrwanda kwa ajili ya kuziba pengo la Geilson Santana JAJA na Said Bahanuzi aliyepelekwa kwa mkopo timu ya Moro United aliyokuwa akiichezea Mrwanda.
Kabla ya kwenda kucheza soka la kimataifa Vietnam na Oman Mrwanda alikuwa amewahi kuzichezea klabu za AFC ya Arusha na Wekundu wa Msimbazi Simba na kufanya vizuri kiasi cha kuzivutia timu nyingi na kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambacho wakati huo kilikuwa kinanolewa na kocha Marcio Maximo.