Suarez aandaliwa mechi za siri Barcelona


Suarez akiwa na mchezaji mwenzake mara tu alipotoka zoezini na klabu ya Barecelona  
In Summary
Kwa kuanzia, Suarez anaweza kucheza katika pambano la kirafiki la leo Jumatatu la Barcelona dhidi ya Leon Guanajuato, hii ni kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya soka nchini Hispania, Guillem Balague.
SHARE THIS STORY
0
Share

ILI aweze kuwa fiti kwa ajili ya pambano la Clasico dhidi ya Real Madrid siku chache baada ya kifungo chake kumalizika, Barcelona inataka kufanya uhuni wa kumwandalia mechi za siri za kirafiki, Luis Suarez, kwa ajili ya kumfanya awe tayari kwa mechi hiyo.
Kwa kuanzia, Suarez anaweza kucheza katika pambano la kirafiki la leo Jumatatu la Barcelona dhidi ya Leon Guanajuato, hii ni kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya soka nchini Hispania, Guillem Balague.
Suarez alifungiwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka (Fifa) kwenye Kombe la Dunia kule Brazil hivi karibuni kwa kosa la kumng’ata beki wa timu ya taifa ya Italia, Georgio Chiellini. Alikuwa akiichezea timu yake ya taifa ya Uruguay.
Matokeo yake, staa huyo wa zamani wa Liverpool alifungiwa kucheza soka kwa miezi minne huku pia akifungiwa kuichezea timu ya taifa ya Uruguay mechi tisa na pia akiambiwa asijishughulishe na lolote kuhusu soka.
Hata hivyo, Alhamisi iliyopita mahakama ya masuala ya kimichezo ilimruhusu Suarez kufanya mazoezi na Barcelona huku pia ikidaiwa kuwa anaruhusiwa kucheza mechi zisizo za mashindano na timu hiyo ya Catalunya.
Balague anaamini kwamba hukumu hiyo itawafurahisha Suarez na Barcelona ambao wanaamini kwamba wanaweza kufanya ujanja ujanja wa kumuweka fiti mchezaji huyo.
Mchambuzi huyo pia anaamini kuwa Barcelona inajipanga kumuandalia Suarez mechi nyingi za kirafiki.
“Naamini kuwa haikuwa sahihi kumzuia asifanye kazi yake kabisa. Hakuweza hata kufanya mazoezi katika uwanja wa soka. Nadhani atatambulishwa rasmi muda wowote kuanzia sasa hasa Jumatatu (leo),” alisema.
“Kuna michuano ya Kombe la Gamper ambayo kwa mujibu wa utamaduni wao inatumika kutambulisha wachezaji wao. Watacheza na Leon na ni kitu wanachofanya kila mwaka. Kuna wazo la kumtumia Suarez.
“Kumekuwapo na mawazo kwamba Barcelona inaweza pia kuandaa mechi nyingi za kirafiki katika uwanja usio na mashabiki na ambao utafungwa milango kwa ajili ya kumfanya acheze mechi nyingi za kumweka fiti.
“Fifa pia bado haijaamua kama Suarez anaweza kuruhusiwa kucheza mechi za kirafiki za Uruguay. Lakini kwa vyovyote vile, lazima Barcelona na wanasheria wa Suarez watakuwa na furaha na hukumu hii.”