Balaa
Daley Blind, anaweza kuwa nje hadi wiki sita baada ya kuumia vibaya goti
lake akiwa katika majukumu ya timu ya taifa lake la Uholanzi juzi
Jumapili.
In Summary
Kiungo mkabaji mahiri wa United, Daley Blind,
anaweza kuwa nje hadi wiki sita baada ya kuumia vibaya goti lake akiwa
katika majukumu ya timu ya taifa lake la Uholanzi juzi Jumapili katika
pambano dhidi ya Latvia waliloshinda mabao 6-0.
Kiungo mkabaji mahiri wa United, Daley Blind,
anaweza kuwa nje hadi wiki sita baada ya kuumia vibaya goti lake akiwa
katika majukumu ya timu ya taifa lake la Uholanzi juzi Jumapili katika
pambano dhidi ya Latvia waliloshinda mabao 6-0.
Blind alianguka katika dakika ya 19 kwenye Uwanja
wa Amsterdam Arena na kukanyagwa na mchezaji wa Latvia, Eduards
Visnakovs. Huyo ni mchezaji wa 39 kupata majeruhi katika kikosi cha
Louis van Gaal tangu alipochukua nafasi klabuni hapo Julai mwaka huu.
Pia ni wastani wa mchezaji mmoja kuumia kila baada ya siku tatu.
Blind aliweza kuondoka uwanjani akitembea
mwenyewe, lakini imedaiwa kuwa atakuwa nje kwa wiki nne hadi sita.
Ingawa vipimo vilitarajiwa kujulikana jana Jumatatu jioni, lakini
inadaiwa kuwa Blind atakuwa nje mpaka Mwaka Mpya.
Blind alitumia mtandao wake wa Instagram
kuthibitisha majeraha hayo akisema: “Najivunia kucheza mechi 25 za timu
ya taifa ya Uholanzi, lakini nimejisikia vibaya kutokana na majeraha
haya.”
Naye kocha wa sasa Uholanzi, Gus Hiddink, alisema:
“Mimi si daktari, lakini nina mtazamo hasi. Goti lake lilikunjika na
inawezekana kuna madhara makubwa. Kesho (jana Jumatatu) kutakuwa na
vipimo maalumu.”
Huo ni mwendelezo wa wachezaji majeruhi katika
kikosi cha United ambacho tayari kinatazamiwa kuwakosa wachezaji muhimu
katika mechi zijazo.
Kipa namba moja, David De Gea, atakuwa nje kwa wiki nne baada ya kuumia kidole akiwa na Hispania Ijumaa iliyopita.
Mabeki wanne wa United wana matatizo. Wakati Phil
Jones akiwa ameumia ugoko, Muargentina Marcos Rojo ameteguka bega,
Rafael Da Silva ana matatizo ya misuli wakati Jonny Evans ameumia
kifundo cha mguu.
Wiki iliyopita, kiungo Michael Carrick alijitoa
katika kikosi cha timu ya taifa ya England kutokana na tatizo la nyonga
wakati Ander Herrera amekuwa na tatizo la ufa katika mbavu.
Mshambuliaji, Radamel Falcao, amekuwa na tatizo la
kiazi cha mguu na anafanyishwa mazoezi maalumu kwa ajili ya kucheza
pambano dhidi ya Arsenal Jumamosi.