Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kafulila
(NCCR Mageuzi) alisema amechukua uamuzi huo kutokana na ubabaishaji wa
makusudi kuiweka wazi ripoti hiyo. “Nasisitiza kwamba fedha za Escrow,
Dola za Marekani 270 milioni, zimetolewa kifisadi na ndio sababu kwa
muda sasa umekuwapo mkakati wa kuzuia ripoti za uchunguzi zisijadiliwe
Bunge lijalo. Wito wangu kwa Serikali, iwapo ripoti hii haitaletwa,
Bunge lijalo halitakalika. Nitapeleka hoja ya kutokuwa na imani na
Serikali,” alisema.
Alisema ni wazi Kampuni ya Ufuaji Umeme ya IPTL na
ya Pan African Power Solution (PAP), zimejipanga kuwapotosha Watanzania
wasijadili masuala ya biashara ndani ya IPTL, wakati mauziano yao yana
utata wenye masilahi ya Taifa kwa kuwa yanaambatana na kodi, hasa
kitendo cha kuripoti kuwa asilimia 70 za hisa za IPTL ziliuzwa kwa Sh6
milioni, ikimaanisha ukwepaji mkubwa wa kodi.
“Ninasisitiza, Singasinga Sethi (Singh Sethi,
Mkurugenzi wa Pan Africa Power Limited) aache kampeni za kupotosha umma
wa Watanzania kwa nguvu ya fedha.
“Mkakati unaoendelea kuhakikisha ripoti haziji
Bunge lijalo, usitishwe mara moja kwa sababu nchi inaumia, hakika
sitakubali agenda niliyoanzisha ihujumiwe,” alisema.
Aliwahakikishia Watanzania kuwa katika suala hilo lazima ‘vigogo’ waliohusika waondolewe. SOURCE>> Mwananchi
