Beki wa kulia wa Simba, Hassan Kessy.
BEKI wa kulia wa Simba, Hassan Kessy, amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhakikisha linamchukulia hatua kali za kinidhamu kiungo wa JKT Ruvu, Nashoni Naftali, baada ya kumdhalilisha.
Jumatano iliyopita, Naftali alimdhalilisha Kessy katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliozikutanisha timu zao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kitendo alichofanyiwa Kessy ni kama kile alichofanya beki wa Mbeya City, Juma Nyosso kwa John Bocco wa Azam FC.
Akuzungumza na Championi Jumamosi, Kessy alisema kuwa, TFF inatakiwa kumchukulia hatua kali Naftali tena zaidi ya Nyosso aliyefungiwa miaka miwili kujihusisha na soka ili liwe fundisho kwake.
“Sina la kuzungumza kwa sababu jamaa aliniudhi sana, ila naomba TFF imchukulie hatua kali za kinidhamu mchezaji huyo ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo,” alisema Kessy.
Alipotafutwa Naftali ili azungumzie suala hilo, hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila ya kupokelewa.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa JKT Ruvu, Ramadhani Madoweka, alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema: “Taarifa hizo za kudhalilishwa kwa mchezaji huyo wa Simba ndiyo kwanza nazisikia kutoka kwako.
“Ngoja tufanye uchunguzi na ikibainika ni kweli mchezaji wetu amefanya hivyo, tutamchukulia hatua, wenye hizo picha tutakapozihitaji tunaomba watupatie ushirikiano wala wasiogope.”
Kwa upande wa TFF, ofisa habari wake, Baraka Kizuguto, alisema: “Taarifa za tukio hilo bado hazijafika kwetu, kama zitafika tutatoa ufafanuzi.”