RAIS DKT. MAGUFULI ATINGA BENKI YA CRDB TAWI LA HOLLAND JIJINI DAR LEO





RAIS DKT. MAGUFULI ATINGA BENKI YA CRDB TAWI LA HOLLAND JIJINI DAR LEO


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amezua taharuki mjini leo baada ya kufika katika Tawi la CRDB (Holland Branch), akiwa kwenye gari binafsi lenye namba T 182 DFQ huku likiwa halina nembo ya adamu na hawa wala bendera.
Tukio hilo lililochukuwa takribani dakika 25, limetokea majira ya saa nne asubuhi ya leo jijini Dar es Salaam katika tawi la benki hiyo ambalo liko katika makutano ya Barabara ya Ohio na Samora bila kutarajiwa.
 Mara baada ya Rais Magufuli kufika katika eneo liliko tawi hilo makutano ya barabara hizo yalifungwa huku ndipo rais aliposhuka kwenye gari  na kuingia ndani ya benki hiyo.



Wakati akikaribia kuingia ndani ilibidi baadhi ya wateja waliokuwa wakijiandaa kuingia ndani ya benki hiyo ilibidi wazuiwe kuingia huku huduma ikiendelea tu kwa wale ambao waliokwisha ingia.
Aidha, baada ya kuingia ndani baadhi ya wateja wa tawi hilo na wananchi wengine walibaki wakishangaa huku wengine wakijiuliza imekuwaje Rais kuingia benki kwa staili ile kwani baadhi ya wananchi kudai kuwa hawajaona tukio kama lile kwa marais wote waliopita.
James Charles, ambaye ni dereva wa Texi, alisema baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye eneo hilo baada ya kuona ulinzi unaimalishwa walishtuka huku wasijue ni nini kinaendelea, hadi pale walipomuona Rais Magufuli akishuka kwenye gari hali iliyowafanya wafikirie anakwenda kutembelea ofisi yake ya zamani.
“Lakini kufumba na kufumbua tukamuona anaelekea kwenye benki ya CRDB tukajiuliza vipi rais leo kaamua kuwa kama mteja hata hivyo hatujui kama hiyo ilikuwa inawezekana. Lazima kutakuwa na kitu haiwezekani aende akachukue fedha kwa utaratibu ule ngoja tusubiri tutasikia amefuata nini,” alisema Charles.
Joyce Godwin ambaye ni mwanafunzi wa chuo kimojawapo cha elimu ya juu, alisema kuja kwake kumewashtua wafanyakazi wa tawi la benki hiyo kwani walidhani alikwenda pale kwa ajili ya kutumbua majipu.
“Mimi wakati Rais Magufuli anaingia nilikuwepo ndani kwenye foleni nikisubiri huduma kwa ujumla kila mmoja wetu alishtuka lakini hatukujua kilichomleta,”alisema.







Baada ya Rais Magufuli kumaliza kazi yake iliyompeleka alitoka na kuingia kwenye gari huku akiwapungia mkono wananchi.Muuza maji (kushoto) akishangaa gari alilopanda Rais Magufuli leo asubuhi wakati akitoka Benki ya CRDB tawi la Holland. Gari alilokuwa amepanda Rais John Magufuli lenye namba za usaji T 182 DGQ likitoka katika benki ya CRDB tawi la Holland lililopo katika makutano ya barabara ya Samora na Ohio jijini Dar es Salaam. Rais John Magufuli akiwa ndani ya gari lenye namba za usajili T182 DFQ huku akiwapungia mkono watu waliokuwa nje ya Benki ya CRDB tawi la Holland jijini Dar es Salaam jana, wakati akitoka katika benki hiyo. (Picha na Francis Dande)
Michuzi