DAR ES SALAAM: Imevuja! Wakati wimbi la wananchi kuingia jijini Dar es Salaam kutoka mikoani na kujiingiza katika kazi ya kuombaomba limekuwa likiongezeka kila siku, watu wanaowapa mimba ombaomba hao wamebainika.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, idadi ya ombaomba katika Jiji la Dar es Salaam imeongezeka maradufu ndani ya muda mfupi, licha ya juhudi za kuwaondoa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa miaka michache iliyopita. Ombaomba wengi wa umri tofauti, wengine wakiwa ni watoto wadogo wanaonekana katika maeneo ya Kariakoo, Mnazi Mmoja, Fire, Posta, Feri, Kinondoni Morocco, Ubungo, Tazara na kwingineko.
Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa baadhi ya ombaomba hao ni wajawazito na wengine wanalea watoto wadogo, licha ya kwamba wengi wao wanaonekana kuwa wadogo kiumri na wanaishi maisha ya kusikitisha.
“Inaonekana hawa vijana ndiyo wahusika kwa sababu wanakuwa pamoja muda mwingi, sasa giza linapoingia, maana hawa ombaomba hawana sehemu maalum ya kulala ndipo wanapochukuliwa kirahisi na kujikuta wanapata mimba,” kilisema chanzo hicho.
“Huu ujauzito mwenyewe yupo, wala siyo hawa machinga. Ni mfanyakazi kwa mtu binafsi, huwa nalala kwake na amesema atanioa,” alisema kwa kifupi binti mmoja mjamzito (17), aliyekutwa Mtaa wa Maktaba, Posta jijini Dar es Salaam ambaye pia alikuwa ameongozana na mtoto mdogo aliyedai hafahamu anakotokea.
“Tukikaa hapa kwa muda huwa tunarudi Dodoma, huko ndiko tunakoshiriki mapenzi na watu wetu, tukipata mimba tunakuja Dar kuendelea kuilea na tukijifungua tunaenda mara moja nyumbani kupeleka watoto,” alisema mmoja wa wanawake hao.
Kwa upande wake, kijana mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Josh anayeuza maji na soda katika mitaa ya Posta, alisema siyo kweli kwamba wao wanawapa mimba ombaomba, kwa sababu wana familia zao na wanatimiza majukumu yao kama kawaida.
“Tunasingiziwa tu bro, sisi giza likiingia tunarudi majumbani kwetu, hawa wenzetu wengi wao wanalala huku mjini, ingawa ni kweli tunakuwa wote mchana kutwa. Waulizeni vizuri, watakuwa wanawajua wanaowapa hizo mimba,” alisema kijana huyo.
OFM bado inafuatilia kwa ukaribu jambo hili ili kujiridhisha lakini wadau mbalimbali waliozungumza na gazeti hili, wameitaka serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inayoongozwa na Ummy Mwalimu, kuchukua hatua za haraka ili kupunguza wimbi la ongezeko la watoto wa mitaani.
Gazeti hili lilipomtafuta Waziri Ummy, simu yake haikuwa ikipatikana hewani.