Aliyemng’ata na Kumtesa ‘House Girl’ Avamiwa na Majambazi


KESI ya kumtesa mfanyakazi wa ndani inayomkabili mkazi wa Mwananyamala, Amina Maige (42), imeahirishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jana kutokana na mshtakiwa kuvamiwa na watu wasiojulikana na kumkata kwa mapanga.

Shauri hilo litakuja tena Juni 16, mwaka huu endapo hali ya mshtakiwa ikiendelea vizuri.




Mbele ya Hakimu Yohana Yongolo, Wakili upande wa Jamhuri ulidai kwamba shauri hilo lipo mbele ya mahakama hiyo kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa ushahidi upande wa mlalamikaji.

Mdhamini wa pili wa mshtakiwa Chausiku Maige, aliiambia mahakama hiyo kwamba Amina ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa alivamiwa na watu wasiojulikana ambapo tukio hilo lilitokea nyumbani kwake Mei 7, mwaka huu.

Mheshimiwa mtuhumiwa kwa sasa yupo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Taasisi ya Mifupa (MOI), akiendelea na matibabu baada ya tukio hilo lililotokea nyumbani kwake alfajiri wakati akitoka ndani kuelekea kazini.

Tulitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Osterbay kisha tulipewa RB/7647/2015. Amina amepata majeraha makubwa sehemu za mkononi pamoja na kichwani,” alidai Chausiku.




Hakimu alimhoji mtuhumiwa huyo kama  eneo analoishi mtuhumiwa huyo ana uhasama na jirani zake, ambapo shahidi huyo alijibu kuwa hajui kwa kuwa haishi naye karibu.

Amina Maige kwa mara ya kwanza alipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo Juni 13, mwaka jana akikabiliwa na tuhuma za kumchoma pasi na kumng’ata mfanyakazi wake wa ndani, Yusta Kashinde (20) hali iliyosababisha maumivu makali mwilini.