Ni mfano wa kirusi kilichokosa jina ambacho kinasambaa na kuathiri wanafunzi wengi wanaofikiria na kuamini kuwa ‘kupiga chabo’ (kuibia katika mtihani), ni njia pekee inayoweza kuwakomboa katika masomo yao.
Siku chache zilizopita, taarifa zilisambaa mitandaoni kuhusu tukio la wazazi 300 waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka nchini India, baada ya kukutwa katika vituo vya kufanyia mitihani, wakitumia njia mbalimbali kuvujisha majibu kwa watoto wao waliokuwa wakifanya mitihani yao ya mwisho.
Wazazi hao walikamatwa baada ya kunaswa na mtego wa kamera ulioonyesha mkanda wa video wa tukio hilo lililotokea katika jimbo la Bihar.
Kutokana na tukio hilo, wanafunzi zaidi ya 700 wamefutiwa matokeo wa mtihani huo ulioandaliwa na Bodi ya Mitihani ya jimbo la Bihar(BSEB).
Hali ilivyokuwa
Waziri wa Elimu nchini India, PK Shai, alisema hali hiyo isingeweza kuondolewa kwa nguvu ya serikali pekee kutokana na ukubwa wa tukio, kwani watu watatu mpaka wanne walionekana wakitoa majibu ya mtihani kwa mwanafunzi mmoja.
Kwa mujibu wa picha zilizosambazwa kwenye mitandao, ikiwamo iliyotumika katika makala haya, wazazi wanaonekana wakiwa katika madirisha ghorofani wakitafuta njia za kuwapa. watoto wao majibu.
Funzo kwa Tanzania
Vitendo vya udanganyifu kwenye mitihani, ni tatizo la kidunia. Kwa Tanzania, wachambuzi wanasema wapo wazazi wanaoshirikiana na walimu na hata wamiliki wa shule kuiba mitihani kwa minajili ya kuzipa shule jina kwa kufaulisha.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Chiungutwa, iliyopo Wilaya ya Masasi vijijini, Hamza Nampoto, anataja sababu tatu zinazosababisha uvujishaji wa mitihani kwa wanafunzi.
Sababu ya kwanza anataja kuwa ni mikataba ya ukuzaji wa viwango vya ufaulu inayotolewa kati ya shule na uongozi wa elimu kama vile wilaya au mkoa. Mikataba hii anasema inawashawishi walimu kufanya udanganyifu kwa sababu za kuwaridhisha wakubwa au kuepukana na adhabu.
“Mwalimu mkuu inabidi atumie namna yoyote ile ili kuhakikisha shule yake inafaulisha ili angalau aweze kufikia kile kiwango alichoagizwa na Mkurugenzi au Katibu tawala wa Mkoa,’’ anasema.
“Kabla ya kuangalia uwezo au uzoefu wa mfanyakazi, mwajiri huangalia zaidi cheti, kwa hivyo inashawishi hata wazazi kutumia mbinu zote kuhakikisha watoto wao wanafaulu.’
Sababu ya pili anasema ni baadhi ya wazazi wanaotaka watoto wao wapande madaraja ya elimu pasina kujali kama wana uwezo au la.
‘’Pia hata mazingira ya rushwa kwa wasimamizi yamekuwa yakitawala, kuna wasimamizi ambao wanaamini kupata nafasi hiyo ni kumaliza shida zao kwa kuuza mitihani,’’anataja sababu ya tatu.
Mzazi Maria Mwemezi, anasema chanzo kikuu cha udanganyifu kwenye mitihani, ni mfumo wa ajira unaopigia zaidi chapuo ubora wa vyeti badala ya maarifa na ujuzi wa wahitimu.
Anasema hakuna ofisi yeyote iliyo tayari kuajiri mfanyakazi asiyekuwa na vyeti vizuri, kama anavyofafanua:
“Kabla ya kuangalia uwezo au uzoefu wa mfanyakazi, mwajiri huangalia zaidi cheti, kwa hivyo inashawishi hata wazazi kutumia mbinu zote kuhakikisha watoto wao wanafaulu.’
Kaimu Mkurugenzi wa shirika la HakiElimu, Godfrey Boniventura, anasema wanafunzi wengi vyuoni hawasomi kwa bidii, bali wanasubiri kuvuja kwa mitihani
‘’Maana ya kwenda shule siyo kutafuta vyeti bora, bali ni kuhakikisha mwanafunzi anapata maarifa ya kutosha, uwezo wa kujiamini katika kazi anayoifanya na mawasiliano ya kujieleza mbele ya watu, ‘’anasema.
Athari ya ufaulu unaotokana na kufanya udanganyifu, anasema ni kuwapo kwa Watanzania katika soko la ajira ambao vyeti vyao havifanani uwezo walionao.
“Unakuta mwanafunzi ana cheti kizuri cha chuo kikuu lakini hawezi hata kujieleza, sasa unajiuliza alipata vipi cheti hicho. Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, bado tunaburuzwa na wenzetu katika soko la ajira ukiacha Burundi inayoshika nafasi ya mwisho, sasa tunaelekea wapi?”anahoji.
Elimu kugeuzwa biashara
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch anasema jambo jingine linalosababisha wizi kwenye mitihani ni ushindani wa shule kufaulisha kwa minajili ya kuvutia soko la wateja (wanafunzi).
“Shule zimekuwa biashara na biashara ni matangazo, ili upate wateja ni lazima ufaulishe sana. Kwa hivyo, inakubidi kutumia mbinu zote kufaulisha kwa kiwango cha juu,” anasema na kuongeza:
“Hata hivyo, kwa miaka mitano sasa sijasikia uvujishaji wa mitihani, kwa sababu Necta wamefunga mianya kwa asilimia zote kwa shule za umma na binafsi.
Anasema shule nyingi zinajitangaza kwa viwango vya ufaulu, hususani katika matokeo ya kidato cha nne na sita. Kutokana na mazingira hayo, wazazi wengi wamekuwa wakishawishika kupeleka watoto katika shule hizo.
Mtazamo wa kitaalamu
Mwaka 2000, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako, alisema mitalaa ya elimu nchini inachangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa udanganyifu katika mitihani.
Alilitazama suala hili kuanzia namna ya uandaaji wa walimu, uelewa wa mitalaa, mazingira ya kufundishia na kujifunzia, menejimenti za shule na pia matarajio ya jamii katika elimu.
Akizungumza katika mkutano wa 20 wa Chama cha Tathmini ya Elimu Barani Afrika (AEAA) uliofanyika mkoani Arusha, Dk Ndalichako wakati huo akiwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kila kipengele kinawachochea wanafunzi, wazazi na walimu kujiingiza katika udanganyifu.
Ufumbuzi wa tatizo
Katika mada yake aliyoitoa kwa wajumbe: Jinsi uwasilishaji mitalaa unavyochochea udanganyifu wa mitihani Tanzania, Dk Ndalichako alipendekeza ili kuhakikisha mfumo wa mitihani unakuwa wa haki, kuna haja ya kuwa na mpangilio mzuri wa mitalaa, mbinu za ufundishaji na mitihani yenyewe.
Pia alishauri kuwapo kwa walimu wazuri, wanafunzi wanaofundishwa vizuri na mazingira mazuri ya kujifunzia.