A to Z ya Mgomo wa Madereva Jana, Ulivyoanza, Vurugu na Mabomu na Mpaka Serekali Kusalimu Amri na Kukubaliana na Madereva


MGOMO wa madereva wa mabasi ya mikoani na baadhi ya mabasi ya usafiri Dar es Salaam maarufu daladala uliofanyika jana, uliambatana na vurugu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kulazimisha askari Polisi kutumia mabomu ya machozi kurejesha hali ya amani.

Awali abiria wanaokwenda mikoa mbalimbali walianza kuwasili katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo tangu alfajiri, tayari kwa safari zikiwemo zinazoanza alfajiri hiyo, lakini walikuta mabasi hayo yakiwa yameegeshwa bila kuwa na dalili za safari.

Ilipofika kwenye saa mbili za asubuhi, abiria waliokuwa wameongezeka katika kituo hicho na baadhi ya watu waliosadikiwa kuwa wapigadebe, walianza kufanya vurugu kuzuia magari binafsi yaliyokuwa yakipita katika barabara hiyo.

Watu hao walikuwa wametanda katika Barabara ya Morogoro, huku wengine wakirusha mawe wakizuia magari kupita katika barabara hiyo.




Katika barabara hiyo, matairi yalichomwa na vijana hao waliokuwa wakifanya vurugu katikati ya barabara, wakizuia magari ya watu binafsi pamoja na yale ya Polisi yaliyokuwa na askari.

Mbagala

Vurugu za namna hiyo zilitokea pia katika eneo la kituo cha mabasi cha Mbagala Rangitatu, ambako makundi ya vijana walikusanyika na kuzuia magari kuingia na kutoka kituoni hapo.

Mabomu ya machozi Kuibuka kwa vurugu hizo, kulisababisha askari walikuwa na mabomu ya machozi, kuyatumia kwa kurusha angani ili kusambaza watu. Katika eneo la Ubungo, abiria waliamua kukimbia huku na kule kunusuru maisha yao kabla ya kurejea kwa hali ya utulivu.

Katika eneo la Mbagala, ufyatuaji wa mabomu ya machozi ulisaidia kurejesha hali ya utulivu kwa muda ingawa baadae fujo zilianza tena na kusababisha polisi nao kuendelea kurusha mabomu hayo mpaka hali ilivyotulia.

Abiria Katika kituo cha Ubungo, wakati vurugu zikiendelea, abiria pamoja na madereva walikuwa wametulia ndani ya mabasi kusubiri hatma ya safari zao huku wengine wakiwa wamekaa pembeni mwa mabasi yao.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti baadhi ya abiria waliokuwa katika eneo hilo, akiwemo Abdala Ally ambaye alikuwa katika basi la Tahmeed akisubiri kwenda Tanga, alisema mpaka wakati huo saa tano asubuhi, alikuwa hajui nini hatma yake kwa sababu hakuna tarifa yoyote aliyokuwa amepewa na uongozi wa basi alilopanda.

Abiria mwingine Mwaimu Kijangwa, alisema hali hiyo inatisha kwani tangu asubuhi walikuwa wakishuhudia vurugu na milio ya mabomu ikiendelea.

Alisema walioko kwenye vurugu nje ni vibaka ambao hawaangalii watoto, wagonjwa wala walemavu na kwamba kwa asilimia kubwa hawana uhusiano wowote na mgomo huo, bali maslahi yao binafsi.

Kijangwa alitetea hatua ya Polisi kupiga mabomu na kusema wanachofanya askari kutumia mabomu ya machozi ni sahihi, ili kutuliza vurugu hizo ambazo zitasababisha maafa zaidi.

Madai ya madereva

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala jijini Dar es Salaam (DARCOBOA), alisema wako ambao hawakuwa na mpango wa kugoma, lakini walipotoa mabasi asubuhi walipigwa mawe wakaogopa kujeruhiwa na kuharibu magari, wakarudisha ndani kwa ajili ya usalama.

Katika kikao kilichofanyika kati ya Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka na madereva hao Ubungo, walilalamikia masharti ya kutakiwa kusoma kila wanaposajili leseni zao za udereva, huku wakitakiwa kulipa ada ya Sh 560,000.

Madereva hao walidai kuwa hawapingi kupata elimu, lakini walihoji wakati wa kusoma nani atalinda ajira yao na wataishi vipi wakati wanategemea kipato kutokana na kazi yao.

Madai mengine, ni kuhusu ada kubwa ya Sh 560,000, ambayo waliitaka Serikali kuwalazimisha wamiliki kulipa ada hiyo. Mengine ni kufanya kazi bila mikataba inayoeleweka, kutolipwa mishahara na wengine kulipwa kwa utaratibu kwa huduma za simu na hivyo kuikosesha Serikali mapato na sheria isiyoeleweka ya muda wa safari.

Waziri

Akizungumza na madereva hao jana katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo, Waziri Kabaka alisema Serikali haina nia ya kuwaumiza madereva wala abiria na hivyo imepokea kwa madai yao na kuahidi kuyafanyia kazi.

Waziri huyo na viongozi wengine walifika hapo saa 6.24 na kuanza kuzungumza na madereva ambao awali walimkataa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova wakidai hawataki kuzungumza nae.

Waziri Kabaka akianza kujibu madai madereva hao, alisema ipo haja ya kutafuta utatuzi wa kudumu wa changamoto zinazowakabili madereva na kwa kuanzia Aprili 18 mwaka huu, uongozi wa madereva hao utakutana na viongozi wa Serikali kujadili mustakabali wa madereva.

“Tumekubaliana kwa maslahi yenu tuwe na kikao kikuu Aprili 18 mwaka huu siku ya Jumamosi ofisini kwangu ili tupate madai yote kwa maandishi, mimi nitasimamia hilo,” alisema Waziri Kabaka.

Waziri Kabaka aliwaomba madereva hao kama wanamuamini, waendelee na kazi wakiamini matatizo yao yatatatuliwa siku ya Jumamosi, lakini wakadai majibu yote wanataka yapatikane hapo hapo kabla hawajaendelea na safari.

“Jana nimeongea na viongozi wenu, nilichogundua ni kwamba mikataba haiko kwa madereva walio barabarani, bali kwa watu wachache tu kwa ajili ya kuonesha kwa maofisa kazi, ili wapate leseni, kwa hiyo madereva hata mkiumia kazini hampati haki yoyote kwa sababu hamna mikataba,” alisema Kabaka na kuahidi kulisimamia suala la mikataba kwa uwezo wake wote.

Alisema katika kutatua tatizo hilo kwa muda mfupi, kuanzia sasa wamiliki wa magari ni lazima waende na madereva katika ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kazi na Majini (SUMATRA) pamoja na picha zao ili kuhakikisha mkataba anapewa dereva mwenyewe.

Aidha Kabaka alisema Wizara ya Kazi na Ajira imeanzisha mfuko kwa watumishi wanaoumia kazini, ambao ni lazima waajiri wawalipie wafanyakazi wao ili wanufaike na mfuko huo.

Katika hoja ya kutakiwa kurudi kusoma Chuo cha Usafirishaji (NIT), Kabaka alisema kusoma madereva hawapaswi kutoa fedha zao mfukoni, ndiyo maana inaandaliwa mikataba ili mwajiri atambue majukumu yake.

Kabaka alisema atarejesha utaratibu wa zamani wa madereva wanapotaka kusajili upya leseni zao, hakutakuwa na suala la kurudi darasani na kulipa ada ya Sh 580,000, kama ilivyo sasa na inavyolalamikiwa na madereva jambo ambalo lilipokewa kwa shangwe na madereva.

Safari zarejea

Baada ya maelezo hayo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Madereva (TTDA), Clement Masanja, aliwatangazia madereva kuendelea na safari zao kwamba Serikali imeahidi kutatua changamoto zao.

“Serikali imepokea matatizo yetu shule imefutwa, tochi barabarani hakuna, na vituo vya ukaguzi tutatumia vya mizani tu, posho na mishahara kitaeleweka Aprili 18 mwaka huu na majibu yasipoeleweka tutaweka ‘segere’ jingine,” alisema.

Mkuu wa Mkoa Said Mecky Sadiki alitoa pole kwa madereva na abiria kwa usumbufu uliojitokeza jana.

Baada ya hapo, mgomo huo ulisitishwa na safari zikaanza saa 7.40 mchana baada ya Serikali kukubali kutatua matatizo yao waliyokuwa wakilalamikia, ikiwa ni pamoja na kuondoa dai lao la kurudishwa shule na kuwaachia huru madereva wote waliokuwa wamekamatwa.

Morogoro

Polisi mkoani Morogoro imewakamata watu saba kutokana na sakata mgomo wa madereva wa mabasi na daladala kwa tuhuma za kuwafanyia vurugu madereva wachache waliokuwa wameamua kuendelea kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema hayo jana, mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kikao cha wadau wa sekta ya usafirishaji mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, aliwataja watuhumiwa waliotiwa mbaroni ni madereva wa bodaboda, daladala, makondakta wa daladala na wauza maji ambao waliamua kuwafanyia vurugu madereva wenzao waliokuwa wakipakia abiria maeneo mbalimbali ya mji wa Morogoro.

Hata hivyo aliwataja waliokamatwa kuhusiana na kufanya vurugu hizo ni Momolege Lucas (24), Mohamed Shaaban (22), Hatibu Onesmo (23), Nelson George (34), Jumanne Juma (30) Victor Costa (24) na Bakari Mohamed (19) wote wakazi wa manispaa ya Morogoro.

Hata hivyo alisema, tayari watuhumiwa hao wameshafikishwa mahakamani kwa makosa ya kuwafanyia vurugu madereva wenzao na kitendo hicho ni cha uvunjifu wa amani na ni kosa la jinai.

Mgomo huo ambao kwa madereva wa mabasi ya mikoani haukuwa na nguvu ulianza alfajiri ambapo mabasi yaliegeshwa kituoni hapo bila ya kuwa na madereva hata hivyo ilipofika saa tatu asubuhi baadhi ya mabasi yalianza kusafirisha abiria na shughuli za ukataji tiketi uliendelea kama kawaida.

Hata hivyo licha ya madereva wa daladala kuendelea na mgomo mpaka saa 9 alasiri , madereva wa pikipiki, bajaji na gari ndogo aina ya Noah walichukua nafasi za daladala kusafirisha abiria kwa kutumia vyombo hivyo vya usafiri kwa kwenda kwenye shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wa baadhi ya madereva waliozungumza na mwandishi wa habari hii jana akiwemo wa basi la kampuni ya Stamili linalofanya safari zake Morogoro- Arusha, Lucas Chonya alisema, mgomo huo umekuja baada ya Serikali kutoa agizo la kuwataka madereva kwenda kusomo kwenye vyuo vya udereva kila baada ya miaka mitatu wanapobadilisha leseni zao.

Hata hivyo alisema, kwa madereva ni vigumu kutekeleza agizo ama utaratibu huo kwani licha ya kusababisha usumbufu , pia kwa madereva wengi hawataweza kumudu gharama za ada kwenye vyuo hivyo vya udereva.

Naye Dereva wa basi la kampuni ya Hood, Daru Dagila alisema, utaratibu wa madereva kwenda kusoma kila baada ya miaka mitatu hauwezi kupunguza ajali za barabarani. Hivyo aliwataka wadau wa sekta ya usafirishaji ambao ni kikosi cha usalama barabarani, Sumatra, Tanroads, Taboa wanapaswa kuwashirikisha madereva katika mikutano mbalimbali ili kujua chanzo halisi cha ajali.

Naye mmoja wa abiria aliyekuwa akisafiri kutoka Moro kwenda Dar , Joyce Muro aliiomba Serikali na wadau wa sekta ya usafirishaji kukaa meza moja na kuzungumza changamoto zao ikiwemo ya ajali za mara kwa mara badala ya kukurupuka kutoa kauli na maagizo ambayo yamekuwa yakisababisha migomo.

Dodoma

Usafiri wa ndani wa mkoani Dodoma uliendelea kama kawaida ingawa mabasi yanayotoka mkoani kupitia mjini Dodoma hayakuingia katika muda unaotakiwa.

Pamoja na hali ya usafiri kuwa shwari Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Usafirishaji wa Njia ya Barabarani (TAROTWU) mkoani Dodoma Lawrence Mwashinga amesema hawautambui mgomo na kwamba wao wanaendelea kusafirisha abiria kama kawaida . Akizungumza kuhusu mgomo wa madereva wa Mabasi yaendayo alisema mkoani hapa Mabasi yote yametoka.

‘’Mabasi zaidi ya 20 yanayofanya safari zake toka Dodoma hadi Dar, Mwanza, Mbeya,Iringa, Tabora, Arusha pamoja na wilayani yametoka kama kawaida’’.

Kwa upande wake Katibu wa chama hicho, Musa Nsese aliitaka Serikali na Wahusika kukaa pamoja na kujadiliana badala ya kufanya maamuzi yanayowaumiza na kuwatia hasara abiria wanaosafiri kuelekea mikoa mbalimbali.

‘’Suluhisho la mgomo ni kuwatafuta Wadau na kukaa meza moja ili kujadiliana na kupata suluhisho kwani wanaoumia ni abiria’’ alisema katibu huyo huku akisisitiza kwamba Mikataba kati ya Waajiri na Waajiriwa inatakiwa iangaliwe kwani wanaoajiriwa wamekuwa wakilalamika kuwa wanyonywa.

Naye Dereva wa basi la Champion linalofanya safari kutoka Dodoma kuelekea Dar, Steven Mauye alisema alikiri kuwa mgomo upo ila huku mkoani hauna nguvu ndio maana mpaka sasa hakuna basi lililotoka Dar es salaam.

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wetu umeonesha kwamba ingawa kulikuwa na mabasi yametoka dodoma kwenda dar, hapakuwepo na mabasi kutoka mikoa ya Singida, mwanza, Kigoma yaliyokuwa yakipita Dodoma na kufanya barabara kuwa tupu kwa kukosa pilikapilika za magari ya kutoka mikoani.

Katika stendi ya Sabasaba usafiri ulikuwapo kama kawaida hukuw enye Noah na Hiace wakisema hawahusiki na mgomo huo.

Na katika stendi ya mji mdogo wa Kibaigwa wasafiri walilazimika kupanda Noah kwenda Dodoma kutokana na kutokuwapo na magari makubwa ya abiria kutoka Dar ambayo hupita mjini hapo kuelekea mjini Dodoma