Vurugu na Matusi Zatawala Kwenye Semina ya Wabunge Kuhusu Sakata la Mahakama ya Kadhi......Wabunge Wegi Wapinga Kuanzishwa Kwa Mahakama hiyo

Mambo magumu yameibuka katika suala la kujadili uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, baada ya kutokea  malumbano makali na vurugu huku idadi kubwa ya wabunge wakiitaka serikali kuuondoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi usiwasilishwe bungeni. 

Wabunge wengi walisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha mpasuko na kuvunjika kwa amani nchini.
Aidha, wamesema suala la Mahakama ya Kadhi linataka kufanywa kama mtaji wa kisiasa kwa baadhi ya viongozi wanaotaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu mwaka huu ili kutafuta kura za Waislamu.




Mvutano huo uliibuka jana wakati wa semina ya wabunge kujadili Muswada wa Sheria mbalimbali wa mwaka 2014 ambao ndani yake kuna  Muswada wa Mahakama ya Kadhi ambao umepangwa kuwasilishwa Aprili Mosi mwaka huu siku ya kuahirisha mkutano wa 19 wa Bunge.
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina, alisema Kamati ya Katiba Sheria na Utawala ilipowaita viongozi mbalimbali wa dini kuzungumzia suala hilo Waislamu walitofautiana katika suala la uteuzi wa Kadhi kufanywa na Mufti Mkuu wa Tanzania na wakataka waelewane kwanza kabla ya suala hilo kupelekwa bungeni.
Alisema katika mkutano huo makundi 11 ambayo hayakubaliana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), walisema Muswada wa Mahakama ya Kadhi uletwe bungeni baada ya kuridhiana kwa sababu hawakubaliani na Bakwata ambalo kiongozi wake ni Mufti Mkuu wa Tanzania.
Walisema maaskofu walisema hawana tatizo na suala la Mahakama ya Kadhi, lakini isiwe na muundo kama wa mahakama nyingine na kwamba mawazo ya waasisi wa Taifa, hawakutaka serikali iwe na dini na ndiyo maana hawakuruhusu mahakama hiyo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Kassimu, alihoji ni kwanini Mahakama ya Kadhi inataka kuundwa na kupewa jukumu Mufti ambaye anatoka Bakwata ambayo ni taasisi binafsi na imesajiliwa na Mamlaka ya Rita.
“Bakwata ni taasisi kama zilivyo taasisi nyingine, haikubaliki, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi suala la Mahakama ya Kadhi ili Waislamu wampigie kura kwa sababu anataka kugombea urais mwaka huu, alisema.
Rukia alisema ni marufuku serikali kuwalazimisha Waislamu kuwa chini ya Bakwata na kwamba Waziri Mkuu, Pinda anafahamu kwa kina suluhisho na mvutano huo wa Mahakama ya Kadhi.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR), Moses Machali,  alisema suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kuingizwa katika mfumo wa mahakama za kawaida inajichanganya na ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema mwaka 2011 Rais Jakaya Kikwete wakati anazindua msikiti wa Gadaf alisema suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi lisihusishwe na serikali kwa sababu wapo watu wengine ambao kila mmoja ana imani yake.
Alisema hatua ya serikali kutaka kuuleta muswada huo wakati bado Waislamu wenyewe hawaelewani ni kuwakosea Waislamu na kwamba inawezekana Waziri alilizungumzia suala hili sababu ya malengo yake ya urais.




Machali alisema kama muswada huu utapelekwa Bungeni itatoa fursa kwa madhehebu mbalimbali kila moja kuanzisha mahakama yake hali itakayoleta machafuko nchini kwa kuwa nchi itakuwa katika mfumo wa mahakama za dini.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema muswada unapendekeza kutambua kitu ambacho mfumo wa sheria za nchi hauna na kwamba uongo unaotumiwa na serikali ndiyo unafanya watu wawe na hofu.
Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM), Ally Kessy, alisema: “Katika nguzo tano za Kiislamu Mahakama ya Kadhi haipo, nguzo sita za imani pia haipo, sasa inakuwaje wanadai kitu ambacho hakitambuliki katika nguzo za kiislamu.”
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi urudishwe ukaboreshwe badala ya kuharakisha kuupeleka bungeni wakati bado una utata hata kwa waislamu wenyewe.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambali Nyangwine, alisema Muswada  wa  Mahakama  ya  Kadhi usimamishwe ukafanyiwe utafiti kwanza kwa sababu ndani ya Waislamu wenyewe hawaelewani.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema Wabunge wasipokuwa makini na suala la Mahakama ya Kadhi, Bunge litaingia katika historia kuvunjika kwa amani.
Selasini alisema serikali iachane na kutoa ‘jini’ lililofungiwa na waasisi Mwalimu Nyerere na Karume na kwamba tukifanya mchezo nchi itabaki katika vipande vipande.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa,  alisema jambo hili litaligawa Taifa na kwamba waasisi hawakuwa wajinga walipokataa serikali isiwe na dini.
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa, alisema nchi inaelekea kubaya kwani msingi wa kuleta Mahakama ya Kadhi ni kutaka kuwachota Waislamu kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Serikali kama imedhamiria kuleta Mahakama ya Kadhi ilete katika utaratibu mzuri, lakini kwa huu utaratibu ni unafiki na mwenyezi Mungu hapendi unafiki, tusiwahadae Waislamu,” alisema.
 Khalifa alisema kwa hali ilivyo muswada huo haujaiva na kwamba usiletwe  bungeni hadi hapo serikali itakapojipanga vizuri.
 Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema),David Silinde, alisema suala la imani siyo la chama cha kisiasa kwani suala la Mahakama ya Kadhi litaipeleka nchi kubaya na inawezekana ikawa ndio mwisho wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mnataka kutuvurugia nchi sababu ya kutafuta kura za Waislamu, kwa hili Waziri Mkuu umechemka sana, nalisema hili kwa sababu wewe Waziri Mkuu ndiye uliyeahidi kuleta bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi,” alisema.
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jafo, alisema yasifanyike masikhala mswaada huyo uwasilishwe bungeni.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM),Mchungaji Lackison Mwanjale, alisema serikali ikajipange upya katika suala la Mahakama ya Kadhi kabla ya kuuleta bungeni muswada kwani bado suala hilo halieleweki kwa jamii.




Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM),Martaza Mangungu, alisema hakubaliani na suala la Mufti kupewa jukumu la kuchagua Kadhi Mkuu wakati Waislamu wengi hawakubaliani na Bakwata ambayo inaongozwa na Mufti.
Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa, alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi wapelekewe wahusika kabla ya kuletwa bungeni ili wajadiliane na kukubaliana mambo ya msingi wanayoona yatawafaa katika uanzishwaji wa mahakama hayo.
 Mbunge wa Igunga (CCM), Dk. Peter Kafumu, alisema serikali imeshindwa kusimamia vizuri suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa kushindwa kuwaelimisha wananchi jambo hilo.
Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahaya Kassim Issa, alisema  Waislamu wanataka Mahakama hiyo kwa kuwa wanakosa haki hivyo serikali iruhusu kuanzishwa kwake.
Pinda: Tutatafakari  Upya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akihitimisha mjadala huo alisema kulingana na maoni yaliyotolewa na Wabunge ameelewa kwamba bado hakuna maelewano miongoni mwa Waislamu wenyewe na pia hakuna uelewa wa jamii kuhusu suala hilo.
Alisema mambo yaliyowasilishwa kuhusiana na muswada huo ni maamuzi ya Bunge Maalum la Katiba na siyo yake, bali anabebeshwa msalaba tu kwa sababu alikuwa anaiwakilisha serikali.
Pinda alisema kutokana na hali hiyo, serikali itakaa kushauriana tena na Spika pamoja na Rais waone wafanye nini katika jambo hilo.
Vijembe  na  Matusi
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, wakati akichangia hoja hiyo alishindwa kuvumulia baada ya baadhi ya wabunge kuingilia mchango wake kwa kumzomea na kusema maneno yaliyomuudhi na kuamua kuwatolewa maneno ya kuudhi (matusi).
Mbunge wa Fuoni (CCM), Said Mussa Zubeir, aliwaita baadhi ya wabunge walikuwa wakimzomea wakati akizungumza kuwa ni ‘wapumbavu’.
Wakati wa majadiliano hayo ilipofika saa 8:17 wakati Mbunge wa Kisarawe, Jafo akiendelea kuchangia kulitokea vurugu ambazo nusura wabunge wapigane huku baadhi yao wakiamua kutoka ukumbini.
Kutokana na kutokuwapo hali ya utulivu ukumbini, baadhi ya askari pamoja na maofisa usalama waliokuwapo nje, walilazimika kuingia ndani kuhakikisha amani haivunjiki.
Spika wa Bunge, Anna Makinda, alituliza  vurugu  ukumbini kwa kuwataka wabunge wawe wavumilivu wakati wenzao wakichangia.
Katika majadiliano wabunge zaidi 30 walichangia na zaidi ya 20 walikataa muswada wa Mahakama ya Kadhi usiwasilishwe Bungeni  siku ya Jumatano wiki hii.
Kabla ya kuanza majadiliano, Mbunge wa  Kuteuliwa, James Mbatia, alitoa hoja kwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja, kwamba wakati wa majadiliano waandishi wa habari wasiwepo ukumbini kwa kile alichoeleza ni unyeti wa jambo hilo.
Hata hivyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini,Kessy, alisema kama waandishi wataondolewa ukumbini naye atalazimika kuondoka huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, akisema hakuna sababu ya kuwaondoa waandishi kwa sababu jambo linalojadiliwa wananchi wanataka kulifahamu kupitia vyombo vya habari.
You might also like