MWANAUME NDIYE MWENYE NAFASI YA KULINDA PENDO!

HABARI wadau wa safu yetu, tupo tena pamoja katika kujuzana jinsi gani maisha ya kimapenzi yalivyo. Leo nitakuwa  tofauti kidogo na mara zote ambazo nimekuwa nikiwasiliana nanyi, kwani mara nyingi nimekuwa nikizungumzia kuhusu nafasi ya mwanamke, kuwa ili iwe hivi, basi afanye hivi na kadhalika.
Maandiko mengi yamekuwa ni kama ya kuonyesha kuwa mwanamke ndiye mwenye dhamana kubwa ya kuamua juu ya penzi au ndoa aliyomo. Ingawa ni kweli kuwa kuna umuhimu mkubwa wa mama kuwa mshirika muhimu katika ndoa, lakini amini usiamini, mwanaume ndiye hasa mwenye kushika turufu ya penzi linalohusika.
Na ninasema hivi hasa kutokana na ukweli ambao nafsi zote mbili zinakubaliana kuwa mwanaume ndiye kichwa cha nyumba. Usemi huu unaweza kuonekana ni mwepesi kama utaangaliwa kwa upande mmoja tu, ambao kimsingi unabeba maana ya uwajibikaji juu ya majukumu ya kuilea na kuilinda familia.
Na unapozungumzia kuhusu jambo hili, akili ya kawaida na haraka, ni juu ya wajibu wa mume au baba katika kuhakikisha familia inapata huduma zote muhimu kama chakula, malazi, matibabu, masomo na kadhalika.
Ni kweli. Lakini maana halisi ya kichwa cha nyumba ni kuwa huyu ndiye kila kitu. Wote tunajua, binadamu anaweza kukosa mikono na miguu, lakini akaendelea kuitwa mtu kwa sababu tu, anacho kichwa. Bila kichwa, kiumbe hicho kitaitwa jina lingine lisilo binadamu.
Uzoefu unaonyesha, uharibifu wa ndoa au uhusiano mwingi wa kimapenzi, huanza kupata msukosuko baada ya baba kuanza kutoka nje ya mstari. Nje ya mstari hakumaanishi kushiriki mapenzi, bali hata kuacha kutekeleza baadhi ya majukumu yake. Baba, kwa sababu zozote, anapozembea au kukataa kulipa ada ya mtoto, ni wazi kuwa atamfanya mama kuanza kuwaza mambo mengi hata yaliyo nje ya uwezo wake.
Lakini hata ile ya mapenzi yenyewe, ni mwanaume ndiye mwenye wajibu mkubwa. Kama baba atakuwa ni mtu mwenye furaha muda wote, litakuwa ni jambo la kushangaza sana kumuona mama akinuna. Yapo makosa madogomadogo ambayo wote huyafanya, wakati mwingine kwa bahati mbaya au kutojua.
Lakini kinachotokea kuharibu hali ya hewa ni kwa mmoja wao kuamua kulichukulia jambo hilo dogo kwa tafsiri yake, lakini kwa ubaya na inakuwa mbaya zaidi kama huyu atakuwa ni mwanaume. Imetokea kwa mfano, mmoja wa wapenzi amekwazwa na tabia ya mmoja wa wazazi wa mwenzake. Katika kulizungumzia jambo hili, yule ambaye wazazi wake wanatuhumiwa, kwa makusudi au kwa bahati mbaya, anaweza kusema; ‘kama huwapendi wazazi wangu basi achana na mimi’.
Hii ni kauli ambayo hakuna yeyote angependa kuisikia, lakini kwa kuwa kulikuwa na mazungumzo yaliyotangulia, ni wazi kuwa kitu kikubwa kinachotakiwa ili kuondoa mzozo, ni busara. Kama mnunaji ni mama, ni rahisi baba kumbembeleza na pengine kwa kutumia mamlaka yake, anaweza kulipooza jambo hilo.
Lakini naona kabisa jinsi gani suala hilo linaweza kuwa kubwa kama baba ndiye atavimba mashavu kwa hasira baada ya kauli kama hii. Na labda ieleweke kuwa siyo nia yangu kutetea nafasi ya mwanaume katika uhusiano wa kimapenzi, lakini kama tunataka mambo yetu kwenda sawa, daima lazima tuwe tayari kukubaliana na ukweli, hata kama unatuumiza.
Kwa hiyo, nimalizie tu kwa kuwasihi wababa, kama wenyewe hawawezi kusoma hapa na kuelewa ujumbe ninaowatumia, basi akina mama waonyesheni hapa wasome, kwamba wao ndiyo wenye nafasi kubwa ya kulilea na kulienzi penzi tulilomo!