Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamanda Mohammed
Mpinga(kulia)akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusiana na
maswala ya usalama barabarani,anaeshuhudia kushoto Mkuu wa kitengo cha
Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia.
__________________
· Ni mafanikio makubwa ya kampeni endelevu ya usalama barabarani
· Uvunjaji wa sheria za barabarani nao wapungua
Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamanda Mohammed Mpinga
amesema katika mahojiano maalum kuwa madereva wameanza kuelewa kuwa
tabia ya kuongea na simu au kutuma na kupokea ujumbe wa maneno (SMS)
wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto ni uvunjaji wa sheria za
barabarani.
Kampeni
hii ya usalama barabarani ya kuwataka madereva nchini kuzingatia sheria
za usalama barabarani ilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mheshimiwa Mathias Chikawe hivi karibuni na sasa imeanza
kuonyesha mafanikio.
“Tangu
kuanza kampeni hii ambayo tayari imefanyika katika mikoa mbalimbali
ujumbe umeanza kuwafikia madereva kwa kuwa wanapokuwa wanatumia simu na
kuwaona askari wa usalama barabarani wanashtuka na kuacha kuzitumia. Hii
inadhihihirisha kuwa wameanza kuelewa kuwa ni kosa kufanya hivyo na
tutazidi kuwapatia elimu na wanaovunja sheria kuchukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria,” alisema Kamanda Mpinga.
Alisema
madereva wakizingatia sheria za barabarani kwa kiasi kikubwa ajali
zinazoendelea kutokea kila siku zitapungua na aliipongeza kampuni ya
Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za serikali
katika kupambana na tatizo hili ambalo limekuwa sugu .
Kwa
upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa
Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia, alisema Vodacom itaendelea
kushirikiana na serikali kuunga mkono jitihada za kuondoa matatizo
kwenye jamii kama lilivyo tatizo hili la ajali ili kuhakikisha wananchi
wanaishi maisha murua na marefu. “Tunatoa rai kwa madereva wote
kuzingatia kauli mbinu ya Wiki ya Nenda Kwa Usalama barabarani mwaka huu
isemayo ‘Maamuzi yako barabarani ni hatma yetu - Fikiri kwanza’.”
Aliongeza
kuwa Vodacom itakuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii athari za
kuendesha gari wakati huo huo unatumia simu ya mkononi kupitia kampeni
ya "Wait to Send" pia itaendelea kuhamasisha madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Alisema
kampeni hii itaendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini ili
ujumbe uwafikie madereva wengi ambako hadi kufukia sasa imeshafanyika
katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Pwani, Morogoro,
Dodoma,Singida na Shinyanga.
Katika
kampeni hizi wafanyakazi wa Vodacom kwa kushirikiana na askari wa
usalama barabarani na wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani
wamekuwa wakifanya uhamasishaji kwa madereva kuacha kuongea na simu
wanapoendesha vyombo vya moto na kuwagawia madereva pete maalum za
kuwatahadharisha kutotuma ujumbe wa simu za mkononi wanapokuwa
wanaendesha vyombo vya moto pamoja na zoezi la kupima madereva kubaini
kama wanatumia vilevi linafanyika ambapo wadereva wanaokutwa
wanaendeshwa vyombo vya moto wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
Baadhi
ya madereva na abiria ambao wameshuhudia kampeni hii ikifanyika
katika sehemu mbalimbali wamesema ni ya muhimu na itasaidia kupunguza
ajali nchini. “Hivi sasa ajali nyingi zinazotokea hapa nchini
zinasababishwa na uzembe wa madereva,kampeni hizi zikiendelea
zitapunguza ajali kwa kiasi kikubwa,” alisema Bi. Zainab Khalfan mkazi
wa Singida.
Naye
James Mshiu mkazi wa Dar es Salaam alilipongeza Jeshi la Polisi na
wadau wa kampeni hii kuwa kwa kiasi kikubwa imepunguza matukio ya ajali
katika msimu wa Krismas na mwaka mpya. “Katika miaka iliyopita
kumekuwepo na matukio mengi ya ajali katika msimu wa sikukuu ya Krismas
na Mwaka Mpya lakini mwaka huu uhamasishaji wa kuzingatia sheria za
barabarani uliofanyika katika kipindi hiki kwa kiasi kikubwa umepunguza
matukio ya ajali za barabarani,” alisema.
Mwisho.