WIVU:Mbongo ashinda Big Brother, Davido apinga


IN SUMMARY
Hilo lilimfanya mshiriki huyu kuonekana ni mtu anayependa wasichana na kukamilisha usemi wake wa siku aliyokuwa akiingia kuwa amekwenda kwa ajili ya wasichana.
MTANZANIA amekuwa gumzo tena. Mataifa yanampongeza, Idris Sultan, kwa kuibuka mshindi wa ‘Big Brother Africa Hotshots 2014’ kwa ushindi wa kishindo ambao alipigiwa kura na nchi tano huku Tayo aliyeshika nafasi ya pili akiambulia kura za nchi mbili tu.
Kwa mujibu wa kura za fainali zilizotolewa na Big Brother, mshiriki aliyepata kura nyingi zaidi ni Idris ambaye alipigiwa kura na Kenya, Namibia, Rwanda, Tanzania na Uganda. Ushindi huo umemwezesha kuibuka na Dola za Marekani 300,000 sawa na Sh522 milioni.
Tayo alipata kura za nchi mbili yaani Nigeria na Msumbiji. Macky 2 alipigiwa na Zambia pamoja na nchi nyingine za Afrika (ROA).
Botswana na Afrika Kusini walimpigia Nhlanhla huku JJ akipigiwa na Zimbabwe, Sipe naye alipata kura moja kutoka Malawi huku Butterphly akitoka kapa.
Idris Sultan ambaye mpaka anaondoka nchini kwenda kushiriki mashindano hayo alikuwa mpiga picha na msanifu kurasa huku akifanya kazi katika kampuni ya I-View Studio, anarudi nchini akiwa na uwezo wa kufungua kampuni yake mwenyewe.
Licha ya ushindi wa kishindo alioupata, maisha ndani ya jumba hilo yalitawaliwa na ‘totoz’ baada ya Mtanzania huyo kuanzisha uhusiano na washiriki wawili; Goitse wa Botswana na Ellah wa Uganda.
Hata hivyo aliwahi kuwa na ukaribu na Samantha, kiasi cha kutungiwa jina la Samdris.
Hilo lilimfanya mshiriki huyu kuonekana ni mtu anayependa wasichana na kukamilisha usemi wake wa siku aliyokuwa akiingia kuwa amekwenda kwa ajili ya wasichana.
Ushindi wake umekamilika baada ya kuishi ndani ya jumba hilo kwa takribani siku 63, tangu yaanze mashindano hayo. Licha ya kuingia na washiriki wengine saba kutokea Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo nchi pekee iliyokuwa imebakiwa na mshiriki wake ndani ya jumba hilo mpaka fainali kabla ya kuibuka na ushindi.
Hata hivyo mataifa mbalimbali yalimuunga mkono Idris kupitia mastaa wa muziki na watu mashuhuri ambao walikuwa wakimpigia kampeni kupitia mitandao ya kijamii.
Kabla ya kuibuka kidedea, Idris alikuwa anaonekana ni mwenye wasiwasi mwingi, huku Tayo kutoka Nigeria akionyesha kujiamini na kuhisi kwamba yeye ndiye mshindi wa usiku huo.
Baada ya kukaa ndani ya nyumba kwa muda wa dakika 30, IK aliwaamuru watoke nje na kuibukia jukwaani ambako waliulizwa maswali kadhaa kabla ya mshindi kutangazwa.
Idris aliyekuwa amevalia suti yake iliyotengenezwa na mbunifu wa Kitanzania, Sheria Ngowi, alikuwa akifurahia video zilizokuwa zikionyeshwa kuhusu maisha yake aliyoishi ndani ya jumba hilo sambamba na vituko kadha wa kadha alivyowahi kuvifanya, ilikuwa hivyo kwa Tayo pia.
IK alimuuliza Tayo iwapo anahisi kuna vitu vimebadilika kwake baada ya kukaa ndani ya jumba hilo kwa siku 63 hizo, walizungumza pia kuhusu ugomvi wake na Idris lakini wote kwa pamoja wakajibu kwamba ni kama maji chini ya daraja na walishayamaliza.
IK akaimba “Mr Loverman, Idris’ akimaanisha kwamba ni mtu aliyekuwa akipenda sana wasichana ndani ya nyumba hiyo, hata hivyo alimsifia kwamba alikuwa mcheshi na aliyeishi na washiriki wenzake vizuri licha ya kukosolewa mara kwa mara.
Akamuuliza Tayo iwapo atapata kuwa mshindi fedha atazifanyia nini naye akamjibu: “Fedha hizi nitampatia mwanamke anayeishi katika nyumba yangu’.”
Swali hilo lilipoelekezwa kwa Idris akajibu: “Nitazirudisha kwa Waafrika”.
Baada ya hapo IK alisimama na kumtangaza mshindi.
“Mshindi wa Big Brother Hotshots ni…. (akawaacha kwa sekunde kadhaa kasha akasema) ni Idrisss...”
Ni historia nyingine
Wakati Idris akiandika historia nyingine baada ya ile ya Richard Deyle Bezuidenhout aliyeibuka mshindi wa msimu wa pili wa mashindano hayo, pia ameendelea kuandika rekodi nyingine baada ya ile iliyoandika na mwanamuziki Diamond Platnumz Novemba 29 jijini Johannesburg baada ya kupata ushindi wa kishindo wa tuzo tatu za Channel O pia usiku wa kuamkia jana Jumatatu pia akiibuka mshindi wa tuzo za Afrima zilizotolewa Nigeria.
Idris ameandika historia pia katika sekta ya burudani nchini, kwa ushindi alioupata ambao unaifanya bendera ya Tanzania ipepee katika mataifa mengi kwa hivi sasa.
Davido azua balaa
Lakini wakati Afrika Mashariki wakishangilia ushindi wa Idris usiku wa kuamkia jana, mwanamuziki wa Nigeria ‘Davido’, alizua balaa baada ya kuandika maneno yaliyowakera mashabiki wa mshindi huyo wa BBA 2014 huo huo baada ya ushindi wa Idris, Diamond aliposti tuzo aliyoshinda Nigeria baada ya matukio hayo kufanyika. Baada ya hapo tena mkali huyo wa wimbo wa ‘Skelewu’ aliposti kitu ambacho kimezua tafsiri tofauti.
Davido aliandika ujumbe mfupi kupitia akaunti yake ya Twitter akidai Watanzania wameiba tena kura kwa mara nyingine ‘N they cheat again lol’ akimaanisha kwamba wamedanganya tena.
Tafsiri ya wadau wa burudani ni kwamba ushindi huo wa Watanzania kwenye matukio tofauti, umewakera Wanigeria akiwamo Davido ambao wanaamini kwamba kuna mbinu kuishusha nchi yao ambao imetawala kwenye burudani muda mrefu.
Posti ya nyota huyo wa ‘Aye’ ilizua mjadala katika akaunti yake ya Twitter hasa baada ya mastaa mbalimbali wanaotokea ukanda wa Afrika Mashariki kuanza kumshutumu kwamba aliyasema hayo kwa kuwa Idris alishinda na si Tayo.
Mastaa hao kutoka Rwanda, Uganda, Tanzania, Kenya, Uganda, Namibia,
Afrika Kusini na hata Zimbabwe, walimjia juu Davido na baada ya dakika kadhaa alifuta ujumbe huo, lakini tayari ulikuwa umepakuliwa na watu wengi. Bado Watanzania wamekua na maswali tofauti kuhusu alichokiandika.
Hata hivyo mashabiki wengi kutoka Nigeria wameendelea kupinga matokeo hayo kwa kudai Big Brother amefanya upendeleo.