SEKTA ya mavazi ni moja kati ya sekta za kiutamaduni ambazo zinazidi kukua kwa kasi huku changamoto kubwa ikiwa ni kulipata vazi la taifa.
Sio suala geni kusikika masikioni mwa watu wakizungumzia upatikanaji wa vazi hilo la taifa kwa kwa kumekuwa na michakato mbalimbali iliyokwishawahi kufanywa na wadau mbalimbali katika kulipata vazi hilo.
Ili kuendeleza utamaduni huo kuna wabunifu mbalimbali ambao kila kukicha wamekuwa wakibuni mavazi kulingana na uhitaji wa soko kwa wakati husika.
Lakini pia
katika kuendeleza utamaduni huo wa upatikanaji wa vazi hilo kumekuwa na
maonesho mbalimbali ya mavazi ambayo yamekuwa yakifanyika sambamba na
kuendeleza utamaduni wa mavazi chini.
Maonesho kama
Lady in Red, Swahili Fashion, Usiku wa Kanga za Kale, Malaika na mengineo yotee
yanalenga kukuza utamaduni huo wa mavazi.
Mbunifu
Evelyn Rugemalila wa Eve Collection anasema kuwa kwa sasa soko kubwa lipo
kwenye nguo za maharusi pamoja na sherehe za Kitchen Party mahsus kwa akina
mama.
Anasema kuwa
kwa upande wake anaona kuwa fursa katika soko hilo ndio inatoa mwanya wa ajira
kwa watu wengi kwa sasa wanaojishughulisha na kazi za ubunifu.
Anasema kuwa
wanadada wengi kwa sasa wanatambua kazi za wabunifu wa ndani na wamekuwa
wakiwatumia katika kuwashone nguo zao za kibunifu.
Anaongeza
kuwa kwa upande wake amekuwa akipata fursa za kuwashonea wanawake wengi hasa
katika hafla mbalimbali.
“Inatakiwa
kuwepo kabisa na sera kwanza ya kulinga hakimiliki ya kazi ya mbunifu wa mavazi
hasa katika kutambua kazi zao, lakini pia inatakiwa kwa wabunifu pia kuzidisha ubunifu
wa kazi ili kuendeleza tasnia hii inayokua kwa kasi hapa nchini”anasema Evelyn.
Ili kuendelea
kuwa na wabunifu wakubwa wa mavazi hapa kama akina Mustapha Hasanali, Evelyn
Rugemalila na wengineo inatakiwa pia kuwepo na mikakati endelevu ya kuwavumbua
na kuwaendeleza wabunifu chipukizi hapa nchini.
Wapo wabunifu
ambao mbali na kuwa na vipaji lakini havijaonekana na kufanyiwa kazi ipaswavyo
na kuwawezeesha kuchangia kikamilifu maendeleo ya tasnia hiyo.
Mratibu Wiki
ya Mavazi ya Swahili Fashion, Honest Arroyal anasema kuwa kupitia wameanzisha
shindano la la kuvumbua vipaji lijulikanalo kama Emerging Designer
Awards.
Anaongeza
kuwa ni katika shindano hilo ambapo wabunifu chipukizi wanaonesha uwezo wao
katika ubunifu wa mavazi na kasha anachaguliwa mbunifu mmoja ambae ndio
anatangazwa kuwa ni mshindi.
Anasema kuwa
chini ya utaratibu kama huo wabunifu kama akina, Martin Kadinda, Pooja Jeshang,
Sara Mosengo Aly Salim wa Mkoto Design na wengineo wamepatikana.
Anafafanua
kuwa kwa mwaka huu ambapo onesho hilo litafanyika Desemba 6, 7 na 8
pia kutakuwa na shindano kwa ajili ya wabunifu chipukizi.
Anaongeza
kuwa hadi sasa wabunifu wengi wameshajitokeza na kuchukua fomu za ushiriki
ikilinganiwa na miaka ya nyuma.
“Najua ili
kukuza utamaduni huu wa mavazi na kuipa tasnia hii heshima inayostahili
inatakiwa kuwepo kwa mikakati ya kisasa kabisa ya kuwaibua wabunifu na Swahili
Fashion ndipo mahala pake”anasema Arroyal.
Kwa upande
wake Martin Kadinda anasema kuwa kupitia maonesho ya mavazi ndipo vipaji vingi
vinaibuliwa na kuwatengenezea mwanya wa ajira vijana.
Anaongeza
kuwa anaona kuwa kwa sasa hata wasanii wamekuwa wakivalia nguo za wabunifu wa
mavazi wa hapa hapa nyumbani.
Anaongeza
kuwa kwa kufanya hivyo inaonesha ni kwa kiasi gani tasnia hiyo ya ubunifu wa
mavazi inahusiana na sanaa ya muziki kwa ukaribu zaidi.
“Kwa mimi
binasfi nilikua nikimvalisha msanii Nasib Abdul, Diamond kwa kipindi kirefum,
na amekuwa akionekana nadhifu tena vema sana, hiyo ni kwa kazi yangu mimi kama
mbunifu wa mavazi”anasema Kadinda.
Anaongeza
kuwa kwa wasanii wa Marekani na kwengineko duniani hali imekuwa ni tofauti kwa
kuwa wao wenyewe wanauza nguo zao na wanapata mabilioni ya fedha.
Hilo
linajidhihirisha kwa msanii mahiri wa Marekani ambae leo anatumbuiza kwenye
Tamasha la Serengeti Fiesta mwaka T.I.
Msanii huyo
anamiliki mavazi yenye lebo mbalimbali kama vile Hustle Gang, Akoo pamoja na
Strivers Row ambayo yameanza kuuzwa kwenye duka la Pop Up Shop lililopo Super
Market ya Dar Free Market.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Grand Hustle Records, Jason Geter ambayo ndio kampuni
inayomsimamia msanii B.O.B na mwanadada anayekuja kwa kasi Iggy Azalea wa
Marekani, anasema
anaamini soko la Tanzania na Afrika kwa ujumla ni masoko makubwa kwa bidhaa
zao.
‘Tuna
matarajio makubwa kuhusiana na kuleta bidhaa zetu nchini Tanzania, na
tunatarajia sio tu kuleta bidhaa zetu hapa nchini, bali kwenda mbali zaidi kwa
kujifunza soko la mitindo hapa nchini’ anasema Geter.
Anaongeza kuwa wasanii
wanatakiwa kutumia umaarufu wao katika kujitafutia vyanzo vingine vya biashara
muhimu.