RIPOTI ya uchunguzi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kuhusu kashfa ya kuchota fedha zaidi ya
sh bilioni 200, kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow zilizohifadhiwa katika
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umeanika madudu mazito yaliyofanywa na
vigogo wa Serikali, Chanzo chetu kimedokezwa.
Ingawa ripoti hiyo ambayo Chanzo hicho
kimebahatika kuiona, imekwepa kutaja majina ya vigogo hao na taasisi
wanazotoka, lakini inaonyesha kuwa jumla ya fedha za Escrow ni sh
bilioni 306 ambazo ni matokeo ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco),
kulipishwa tozo la uwekezaji zaidi ya kiwango kinachotakiwa kulipwa.
CAG katika ripoti hiyo, anasema Tanesco
walipaswa kurejeshewa sh bilioni 321 zilizolipwa ziada kwa IPTL kati ya
mwaka 2002 – 2012.
“Hivyo fedha za Escrow ni fedha za umma,
yote ilipaswa kurudi Tanesco na shirika kuendelea kuwadai IPTL sh
bilioni 15,” alisema CAG.
| Pichani ni wa kwanza James Rugemalira, ambaye alikuwa akimiliki asilimia 30 ya IPTL,na ndiye alikuwa akiwahonga viongozi mbalimbali picha na Maktaba |
Madudu mengine yaliyoibuliwa katika
ripoti hiyo ni kwamba, kampuni ya PAP haikununua kihalali hisa 70% za
kampuni ya Mechmar katika IPTL kwani zilizuiwa na Mahakama, hivyo hawana
hati halisi za hisa na PAP ilifanya udanganyifu katika malipo ya kodi
kwa kutoa nyaraka za uwongo na kuikosesha Serikali Mapato ya sh bilioni
8.7.
Inaeleza kuwa, kosa hili linahusu pia mamlaka ya TRA Ilala, ambao walihusika kufanya mauzo hayo.
Akaunti ya kampuni ya VIP Engineering
and Management (VIPEM), ilifunguliwa na mmoja wa wabia wa IPTL, James
Rugemalira, ambaye alikuwa akimiliki asilimia 30 ya IPTL huku kampuni ya
Mechmar Bhd ya Malaysia ikiwa na hisa asilimia 70.
Kutokana na kiasi hicho cha hisa,
Rugemalira amelipwa kiasi cha dola milioni 75 (Shilingi Bilioni 123),
zikionyesha kwamba alilipwa kiasi cha dola milioni 7.5 (Shilingi bilioni
12.4) mwaka jana na kiasi kilichosalia alimaliziwa mwaka huu.
Kiasi hicho cha fedha kililipwa kwa
Rugemalira na kampuni ya PAP inayomilikiwa na Harbinder Singh, ambaye
kwa sasa ndiye mmiliki pekee wa IPTL baada ya kununua hisa za Mechmar na
zile za VIP.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo Gazeti
hili imeinasa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na
Gavana wa Banki Kuu (BoT), na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, walivunja
sheria kwa kuelekeza kuwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye tozo la
uwekezaji isilipwe na kusababisha serikali kupoteza mapato ya sh bilioni
21.
“Waziri kwa kushirikiana na Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati na Madini, hawakufanya utafiti wa kini kuhusu uhalali
wa umiliki wa kampuni ya IPTL. Katibu Mkuu alisaini kutoa fedha za
Escrow bila kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi, hivyo kusababisha
upotevu wa zaidi ya sh bilioni 321,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa upande wa Tanesco, Mkurugenzi wa
Shirika hilo na Bodi yake, hawakutimiza wajibu wao kwa kugeuza maamuzi
yao (ama kwa kushinikizwa na Wizara au kwa rushwa), na kulikosesha
shirika hilo zaidi ya sh bilioni 321.
Wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda akikaririwa bungeni kwamba fedha hizo sio za umma, ripoti hiyo inaonyesha kuwa ni za umma.
Mgogoro uliosababisha fedha kuwekwa
katika akaunti hiyo ya Tegeta ya BoT, ulitokana na Tanesco kugoma kulipa
gharama za uwekaji mitambo (Capacity Charge), kwa IPTL mwaka 2006 kwa
vile ilibainika IPTL ilikuwa ikitoza gharama kubwa kuliko iliyopaswa.
Akaunti hiyo ya Tegeta, ilianzishwa kwa
sababu ya kuhifadhi fedha zote zilizopaswa kulipwa na Tanesco hadi hapo
mgogoro baina ya pande hizo mbili umalizike.
Hata hivyo, Septemba mwaka jana,
serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, iliagiza BoT kulipa fedha
hizo kwa kampuni ya PAP mara baada ya kuridhishwa na uamuzi wa Mahakama
Kuu uliosema kwamba mgogoro baina ya wamiliki wa IPTL na Tanesco
umemalizika na hivyo Benki Kuu haina sababu ya kuhifadhi fedha hizo
tena.
Uamuzi huo wa kulipwa, ulizua upinzani
mkali bungeni ambapo wabunge wawili wa kambi ya upinzani; Mbunge wa
Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na Mbunge wa Kigoma
Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, walidai kuwa zoezi hilo limejaa
ufisadi na Bunge liliazimia kwamba suala hili lifanyiwe uchunguzi wa
kina na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
pamoja na ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Chanzo Gazeti Makini la Tanzania Daima