Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
wa tatu kutoka (kushoto) Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto,
(kushoto kwake) Makamu wa Rais kwanza wa Burundi, (kulia kwake)
wakijumuika kwa pamoja na viongozi wengine wakionyesha Taarifa ya pamoja
waliyoisaini kuhusu majadiliano ya kuimarisha Miundombinu kwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika mkutano wa 3 wa Wakuu
wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC) kuhusu Miundombinu, uliofanyika kwenye
Ukumbi wa KICC, jijini Nairobi jana Novemba 29, 2014. Picha na OMR.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiongozana na baadhi ya viongozi wakati wakitoka kwenye Ukumbi wa
mikutano wa KICC, baada ya kushiriki katika mkutano wa 3 wa Wakuu wa
Nchi za Afrika Mashariki (EAC) kuhusu Miundombinu uliofanyika jijini
Nairobu, Kenya jana Novemba 29, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
kifurahia jambo na Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto na Waziri wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta, wakati wakiondoka katika viwanja vya
Ukumbi wa mikutano wa KICC, baada ya kushiriki kwenye mkutano wa 3 wa
Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC) kuhusu Miundombinu, uliofanyika
jijini Nairobi, Kenya jana Novemba 29, 2014. Picha na OMR
wengine walioshiriki katika mkutano huo.
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AIWAKILISHA TANZANIA
KATIKA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI (EAC) KUHUSU
MIUNDOMBINU JIJINI NAIROBI, KENYA
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Mohammed Gharib Bilal jana Novemba 29, 2014 aliiwakilisha Tanzania
katika mkutano wa siku moja wa Wakuu wa Nchi zinazounda Jumuiya ya
Afrika Mashariki jijini Nairobi, Kenya. Mkutano huo, kwa mujibu wa
utaratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unafanyika kila baada ya miaka
miwili na lengo lake kuu ni kufanya tathmini juu ya miradi ya
miundombinu inayoshirikisha nchi washirika, sambamba na kutazama fursa
ya kutanua miundombinu mipya katika nchi hizi kwa lengo la kukuza uchumi
wa pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki.
Tathmini hii ya Miundombinu inafanyika kwa kuwa mataifa ya Afrika
Mashariki yanatambua umuhimu wa kuwa na miundombinu bora katika nchi
hizi ili kuharakisha ukuaji wa uchumi, sambamba na kutanua mtengamano wa
nchi hizi na hivyo kuwafanya wananchi wanaoishi ndani ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki kuzidi kuwa wamoja.
Mkutano wa jana uliongozwa na Kaimu Rais wa Kenya Mheshimiwa William
Ruto na kuhudhuriwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal, Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Burundi, Waziri Mkuu wa Rwanda pamoja na Waziri wa
Afrika Mashariki wa Uganda. Viongozi wengine waliopata nafasi ya
kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa Balozi Richard Sezibera,
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mwenyekiti wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Waziri wa Wizara hiyo kutoka
Tanzania, Mheshimkiwa Samwel Sitta, Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika, Dkt. Donald Kaberuka, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Ukanda wa
Afrika, Bwana Makhtar Diop, Katibu Mtendaji wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa
Kituyi na Baalozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Balozi Filiberto
Sebregondi. Pia mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi za
China, Marekani, Japan na nyinginezo ambazo ni wadau wakubwa wa ujenzi
wa miundombinu katika nchi za Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Kaimu Rais wa Kenya,
William Ruto alifafanua juu ya umuhimu wa kuhakikisha Afrika Mashariki
inaunganishwa kwa miundombinu imara ili kukuza uchumi na akapongeza
jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kufanikisha azma hiyo huku pia
akiomba nchi wanachama wa Afrika Mashariki kuendelea kuungana katika
kutekeleza miradi ya miundombinu na kujitahidi kutafuta fedha kwa ajili
ya kukamilisha miradi hiyo.
Mkutano huu pia uliambatana na kupokea ripoti ya utekelezaji wa maagizo
ya Wakuu wa Nchi za EAC kuhusu Miundombinu kutoka kwa Mawaziri wa Nchi
za Jumuiya. Wakuu wa Nchi katika Mkutano huu walipokea taarifa ya
utekelezaji wa maagizo waliyoyatoa katika mkutano wa pili uliofanyika
mwezi Novemba, 2012 na kuidhinisha miradi 72 ya miundombinu ya
kipaumbele ya Barabara, Reli, Nishati na Bandari.
Kwa upande wa utekelezaji; miradi 16 imekamilika, 39 inaendelea
kutekelezwa na 17 ipo katika hatua za awali za kutafutiwa fedha kwa
ajili ya utekelezaji wake.
Kwa upande wa Tanzania miradi minne imekamilika ambayo ni Umeme katika
mji wa Kibondo, mradi wa barabara ya Mbezi-Shule-Tangibovu-Makutano ya
Nelson Mandela na barabara ya Tabata. Barabara nyingine iliyokamilika ni
Nyangunge – Musoma – Sirari na sehemu ya Simiyu - Musoma inayounganisha
Kenya na Tanzania huko ujenzi unaendelea.
Akizungumza katika Mkutano huo Makamu wa Rais amezitaka nchi wanachama
kuharakisha utekelezaji wa miradi ya Miundombinu ili kusaidia
utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja, ambayo inalenga kurahisisha
usafirishaji wa bidhaa na abiria. “Tusiishie kubakiza mipango hii katika
karatasi, tusiishie kuzungumza tu bali huu ni wakati wa kuhakikisha
tunarahisisha ufanyaji biashara katika nchi zetu na kupunguza vikwazo
visivyo vya lazima,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais pia aliambatana na
Mheshimiwa Dkt. Mahadhi J. Maalim, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara wa
Zanzibar, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui. Mheshimiwa Makamu wa Rais na
msafara wake tayari wamerejea nyumbani Tanzania ambapo kesho anatarajiwa
kuwa Mgeni Rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi
Duniani, maadhimisho yanayofanyika Kitaifa Mkoani Njombe.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Novemba 30, 2014