UKOSEFU WA AJIRA KWA VIJANA ULIVYOTENGENEZA ‘BOMU’


Mheshimiwa Abdul Jabiri Marombwa
Rufiji ni moja kati ya wilaya sita za Mkoa wa Pwani ambayo ndani yake, kunapatikana Jimbo la Uchaguzi la Kibiti linaloongozwa na Mheshimiwa Abdul Jabiri Marombwa (54), kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa upande wa Kaskazini, Wilaya ya Rufiji na Mkuranga, upande wa Mashariki kuna Bahari ya Hindi, Kusini kuna Mkoa wa Lindi na upande wa Magharibi, inapakana na Mkoa wa Morogoro.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi lilifunga safari mpaka jimboni humo na kuzungumza na wananchi walioeleza matatizo yao, kubwa likiwa ni vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na makundi ya vijana wanaoshinda vijiweni wakivuta bangi kutokana na kukosa ajira.
MATATIZO YA WANANCHI
Wananchi wa Kata za Bungu, Kibiti, Kiongoroni, Mbuchi, Mchukwi, Utete na nyingine kadhaa, waliliambia Uwazi kwamba matatizo yanayowakabili ni mengi yakiwemo ukosefu wa huduma bora za kijamii kama uhaba wa dawa hospitalini na kwenye vituo vya afya, uhaba wa walimu, vifaa vya kufundishia, vyumba vya madarasa na maabara.
Ukosefu wa miundombinu bora kama barabara zinazopitika misimu yote, maji safi na salama, ukosefu wa umeme kwenye baadhi ya maeneo, kukosekana kwa soko la uhakika la mazao likiwemo korosho, ukosefu wa ajira na vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na baadhi ya vijana wanaoshinda vijiweni, ni matatizo mengine yaliyoelezwa na wananchi wa Kibiti.
“Kuna makundi mengi ya vijana wanaoshinda vijiweni wakivuta bangi, kwa kweli wanatusumbua sana na kutukosesha amani sisi wananchi. Kwa mfano jirani na Sekondari ya Kibiti, Mtaa wa Mbebetini kuna kundi la vijana pale wanakusanyika kwa wingi na kuvuta bangi na kunywa pombe haramu ya gongo, wakitoka hapo wanaanza kusumbua raia kwa kuwakaba, kuwaibia na wakati mwingine kuwabaka wanawake.
“Polisi wanawajua lakini hakuna anayethubutu kwenda kuwakamata mpaka kutokee matukio makubwa kama lile la mwaka jana kiongozi wao alipopigwa na kudaiwa kuuawa na polisi, angalau kidogo waliweza kuwadhibiti lakini kazi haikuwa ndogo kwani ni wengi sana. Tunaiomba serikali itusaidie,” Juma Mtanda, mkazi wa jimbo hilo aliliambia Uwazi.

MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kusikia upande wa wananchi, Uwazi lilimtafuta mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Marombwa ambaye alianza kwa kutoa ufafanuzi kuhusu suala la elimu.
“Miaka kumi iliyopita, jimboni kwangu kulikuwa na shule mbili tu za serikali, Kibiti na Mahege lakini tangu nimeingia madarakani, nimewezesha kujengwa shule 11 ambazo zote zina walimu wa kutosha labda upungufu ni kwenye walimu wa masomo ya sayansi, jambo ambalo bado nalihangaikia kila siku.
“Tatizo kubwa ni jografia ya jimbo langu, kata nne zote zipo baharini, kuna baadhi ya maeneo kama Delta, mwalimu analazimika kutembea kwa miguu na kupanda mtumbwi kwa zaidi ya saa nane kwa hiyo ili kuwapa motisha walimu, shule zimejengwa kwenye maeneo ambayo yanafikika kwa urahisi.
“Kuhusu suala la afya, nimejitahidi katika kila kitongoji jimboni kwangu, nimejenga zahanati. Kipindi cha nyuma, wanafunzi na wananchi wengi walikuwa wakifa kwa ajali za mitumbwi wakati wakihangaika kutafuta matibabu kwa hiyo angalau hilo tatizo limepungua kwa sasa.
“Kuhusu suala la ukosefu wa ajira, ni kweli kuna kundi kubwa la vijana jimboni kwangu hawana ajira.
“Wananchi wangu wengi hawajasoma kwa hiyo ajira pekee inayowafaa ni kilimo. Miaka ya nyuma, walikuwa wakilima minazi lakini kwa miaka ya karibuni, minazi yote imekufa.
“Kwa jitihada zangu binafsi, nimeanzisha mradi wa michikichi, nagawa mbegu bure kwa wananchi wote na japokuwa tupo kwenye hatua za mwanzo, ni matumaini yangu kwamba ndani ya kipindi kifupi kijacho, vijana wote wanaoshinda vijiweni wakivuta bangi, watakuwa wanajishughulisha na kilimo cha kibiashara cha zao la michikichi.
Hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kumaliza tatizo la ukosefu wa ajira jimboni mwangu,” alihitimisha mbunge huyo ambaye ili azifikie kata zote jimboni kwake, ni lazima atumie usafiri wa boti ambapo humchukua siku kumi kulizungukia jimbo lote kwa mara moja.
source>>> Amani