PHIRI AFANYA UAMUZI MAGUMU



KOCHA Mkuu wa Simba Partick Phiri amefanya uamuzi mgumu katika kikosi chake kwa kumweka benchi nahodha na beki mzoefu wa timu Joseph Owino kwenye mechi dhidi ya Stand na sasa amesisitiza lazima akae kikao na mchezaji mmoja baada ya mwingine.
Akizungumza na Mwanaspoti akiwa na machungu ya matokeo ya sare yanayoikumbuka timu yake Phiri alisema kwa sasa ni wazi kwamba anafanya kazi katika mazingira magumu ya kuwa na presha ambapo hajajua kiini cha tatizo linaloimaliza timu yake.
Phiri amepanga kuwapa wachezaji mapumziko ya siku mbili na mara baada ya kurudi kambini anataka kufanya kikao tofauti na kila mchezaji na wasaidizi wake kwa nyakati tofauti.
Alisema kuanzia keshokutwa Jumatano timu yake itakuwa na wiki mbili nzito za kujiimarisha kwa maandalizi ya nguvu kujiweka sawa kabla ya kuwavaa wapinzani wao wa jadi Yanga ambao ametamka kwamba wanazidi kuimarika kadri ya siku zinavyosonga huku wao wakidhoofika.
“Simba ni timu kubwa haiwezi kuzoea hali hii, siyo heshima yake, nimekaa hapa kwa muda mrefu katika nyakati tofauti lakini hali hii haijawahi kunitokea na mpaka sasa sijaelewa nini kiini cha haya matokeo ambayo yanamuumiza kila mmoja anayeipenda timu hii,”alisema Phiri.
“Ukiangalia mazoezi yetu wachezaji wanajituma kwa hali ya juu sana lakini unapokuja kwenye mechi hali inakuwa mbaya sana, tunafunga goli lakini linarudi kwa haraka sana ni lazima nikutane na mchezaji mmoja mmoja na wasaidizi wangu pia kila mmoja kwa wakati wake tusaidiane kujua tunakosa wapi.
“Hatuwezi kucheza na Yanga tukiwa katika hali hii ni lazima tujipange vyema ukiwaangalia Yanga utagundua kwamba ni timu inayoimarika kila wanapoamka huku sisi tukinyong’onyea. Lazima tuamke tutakuwa na wiki mbili ngumu kabla ya mchezo huo,”alisisitiza Phiri.