DI MARIA ADAI AMEWASHTUKIA MABEKI WA ENGLAND


KUSAJILIWA kwa pesa nyingi ni kitu kilichowatoa kijasho Robinho, Andriy Shevchenko na Fernando Torres na kushindwa kufanya kweli kwenye timu zao mpya, lakini staa wa Manchester United, Angel Di Maria amesema hilo haliwezi kutokea.
Winga huyo Muargentina ametua Old Trafford kwa ada ya uhamisho ya Pauni 60 milioni na wakati sasa akikabiliana na kipindi cha kuzoea mazingira mapya ikiwamo lugha ya Kingereza, Di Maria alisema atatuliza daruga zake na kuwa tishio kwenye ligi hiyo.
Licha ya kufunga mabao safi kwenye mechi dhidi ya Queens Park Rangers na Leicester City, Di Maria alisema ameshatambua ugumu wa mabeki wa Ligi Kuu England na tabia zao za kuwachezea rafu washambuliaji wenye vipaji vya kuuchezea mpira.
Di Maria hataki kimtokee kilichomtokea Mesut Ozil msimu uliopita ambapo alianza kwa kasi kabla ya kuchoka na kuonekana hana jipya mwishoni mwa msimu.
“Nimeshaelewa soka la kutumia nguvu nyingi linalochezwa kwenye ligi hii ni tofauti na ilivyo kwa La Liga,” alisema Di Maria.
“Wachezaji wa hapa wanatumia nguvu sana na wanafanya hivyo kila mechi. Nataka kuzoea mazingira.”