Wiki iliyopita niliishia pale nilipokueleza msomaji wangu kuwa makala haya ni ya maisha yangu halisi nimeandika kwa lengo la kukuhamasisha na kukufanya usikate tamaa katika haya maisha kwani hata mimi nimepitia changamoto mbalimbali lakini nikafanikiwa kwa namna ambavyo Mungu amenijaalia, pia nilikuahidi kukusimulia kuhusu uhusiano wangu na Mwanamuziki wa Kenya, Cecilia Wairimu ‘Amani’.
ENDELEA…
“Kabla ishu yangu na Amani niliwahi pia kushiriki kwenye Filamu ya Girlfriend filamu iliyoakisi maisha halisi ya muziki na katika filamu hiyo ilikusanya wasanii na watayarishaji kibao akiwemo Khaleed Mohamed ‘TID’, Gwamaka Kaihula ‘King Crazy GK’, Juma Mohamed ‘Jay Moe’, Ambwene Yessaya ‘AY’, Yvonne Otieno ‘Monalisa’ , Beatrice Morris ‘Nina’, Sultan Tamba na wengine kibao.
“Baada ya filamu hiyo sijawahi kufikiria kufanya filamu nyingine ila sauti na image yangu imekuwa ikitumika kwenye makampuni na kampeni mbalimbali za ndani na nje.
“Nilikutana na Amani mwaka 2005 na kuwa marafiki na baadaye tukawa wapenzi, tulipendana na kuheshimiana ila mwaka 2007 ndipo tuliachana ingawa si kwa ugomvi wala kukorofisha kwa namna yoyote ile sema umbali na gharama ndo vyanzo vya kuachana kwetu, si mimi (AY) wala Amani aliyekuwa tayari kuhamia kweye nchi ya mwingine na ninadhani hii ni kutokana nakuwa wazalendo wa nchi zetu.
“Kila mtu anaipenda nchi yake, Amani humwambii kitu kuhusu Kenya yake, anaipenda sana, mimi pia najivunia kuwa Mtanzania wa kuzaliwa.
“Maisha yaliendelea kama kawaida ila nitabaki namheshimu Amani na maamuzi yake pamoja na maisha yake ya mpenzi au mume mwingine. Katika muda wa uhusiano wangu na Amani, alinifundisha jinsi wanawake wa Kenya walivyo na misimamo iliyonyooka katika mambo yao namkubali Amani kwani hakuwahi kuchanganya biashara na starehe.
“Baada ya kuachana na Amani, nilianzisha uhusiano na mtoto wa mwanamitindo, Asia Idarous anayeitwa Dida Idarous ambaye tulidumu kwa miaka kama miwili hivi tukaachana kwa sababu ambazo binafsi naamini ili muwe wapenzi au wanandoa ni lazima kuwe na mambo ambayo mnaendana kimtazamo na vinginevyo.
“Ukiachana na uhusiano bado niliendelea kufanya kazi zangu kama kawaida na kufanya vizuri na kufanikiwa kufanya shoo nchini za Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Dubai, India, Afrika Kusini, Malaysia, Urusi, Uingereza, Marekani na kwingineko.
“Nashukuru sana Mungu maisha yalisonga kama kawa na hatimaye nilifanikiwa kuanzisha Kampuni ya Mkasi ambayo huzalisha vipindi vya televisheni, matangazo na vinginevyo ila kwa sasa tuna kipindi cha Mkasi ambacho huwa kinaendeshwa na Mtangazaji Salama Jabri kila siku ya Jumatatu, kupitia East Africa Televisheni (EATV).
“Pamoja na mafanikio hayo ambayo Mwenyezi Mungu amenijalia sijafanikiwa kupata mtoto hata wa kusingiziwa na hii ni kwa sababu ya maamuzi yangu binafsi ila kama nikifanikiwa kuwa na familia basi natamani kupata watoto wawili tu ambao nitaweza kuwapa maisha bora