EWURA yapandisha Mafuta kwa Ongezeko la Wastani wa Shilingi 200 Kwa Lita






Kumekucha watanzania na wapiga kura wa nchi hii.Wakuu wa EWURA huku wakiwa na nyuso za bashasha kana kwamba wanatangaza jambo jema,wametangaza Bei mpya ya nishati ya mafuta.

Mafuta yamepanda kwa wastani wa TShs 200 kwa lita.Sababu kubwa ikiwa na kupanda kwa dola.Wachumi mtuambie hii italeta madhara makubwa kiasi gani kwa mtanzania wa kawaida.

--------------------------

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI KIKOMO ZA MAFUTA AINA YA PETROLI KUANZIA JUMATANO, TAREHE 1 JULAI 2015

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini.

Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Tarehe 1 Julai 2015. Pamoja na kutambua bei kikomo za bidhaa mbalimbali za petroli nchi nzima, ni muhimu kuzingatia yafuatayo:-

(a) Bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote yaani Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 3 Juni 2015.

Kwa Mwezi Julai 2015, bei za rejareja kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka kama ifuatavyo: TZS 232/lita sawa na asilimia 11.82 TZS 261/Lita sawa na asilimia14.65 na TZS 369 /lita sawa na asilimia 22.75 sawia.

Kwa kulinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla kwa mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa nazo zimeongezeka kama ifuatavyo: TZS 232.35/lita sawa na asilimia 12.49 TZS 261.15/lita sawa na asilimia 15.57 na TZS 369.41/lita sawa na asilimia 24.32.

Mabadiliko haya yametokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, kuendelea kudhoofu kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani pamoja na mabadiliko ya tozo za Serikali katika mafuta kuanzia mwezi wa Julai 2015.

Kwa kulinganisha thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani kwa machapisho ya bei za mwezi Juni na Julai 2015, Shilingi ya Tanzania imepungua thamani kwa TZS 175.11 kwa dola ya Marekani sawa na asilimia 8.65.

(b) Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.




Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.

(c) Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 7 la tarehe 4 Machi 2015.

(d) Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika.

(e) Wanunuzi wanashauriwa kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita. Stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo; ama endapo utakuwa umeuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.