KIGOGO MAMLAKA YA USALAMA WA USAFIRI WA ANGA (TCAA) AHOJIWA--->>>





 
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili Jaji Mstaafu, Hamis Msumi (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wenzake.
Dk. James Benedict akipangua hoja zilizotolewa na watu wa tume (hawapo pichani).
...Akitoka katika chumba cha mahojiano.
...Akiwa katika lango kuu la Ukumbi wa Karimjee.
...Akijitetea huku wajumbe wa tume wakimfuatilia kwa umakini.
KIGOGO mmoja kutoka Mamlaka ya Usalama wa Usafiri  wa Anga (TCAA) Dk. James Benedict,  leo amehojiwa na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam inayoendelea kuwahoji baadhi ya viongozi wanaohusishwa na sakata zima la fedha za Escrow.
Katika mahojiano hayo yanayofanyika mbele ya mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, ofisa huyo alikuwa kizimbani kuhusiana na  Sh. Milioni 80 alizoingiziwa na ofisa wa kampuni ya VIP, James Rugemalira katika benki ya Mkombozi.
Katika mahojiano hayo ilielezwa kigogo huyo awali ya hapo katika kipindi cha kuingiziwa fedha hizo alikuwa meneja mkuu wa Mamlaka ya Nishati  na Maji (Ewura) kama mtumishi wa umma.
Tume hiyo ilimhoji mtuhumiwa kama anatambua kuwa (Ewura) ni taasisi ya serikali inayojihusisha na nishati na James Rugemalira aliyemwingizia fedha ana hisa katika kampuni ya IPL.
Mtuhumiwa alijibu kuwa anfahamu suala hilo na kuelezwa kuwa katika sheria ya watumishi wa umma hairuhusiwi kupokea kiasi cha fedha zaidi ya sh. 50,000 na kupokea sh. Milioni 80  tayari ulikuwa ni uvunjifu wa sheria ya kanuni zinazowazuia watumishi kupewa fedha na mtu binafsi ama kampuni lolote.
Tume pia ilimhoji Dr. Benedict sababu ya kupewa fedha hizo pasipo kumfanyia kazi yoyote na mtuhumiwa alisema alipewa fedha hiyo kwa ajili ya tiba ya mkewe na hakuona sababu ya msingi kuandikishana kwa maelezo.
Aliulizwa pia kwa nini fedha hiyo iliyoingizwa katika benki ya Mkombozi mnamo Fenruari na Machi 2014 na ilitolewa wakati huohuo  kwenda kulipia nyumba huko Mbezi-Kawe.
Mtuhumiwa alisema alikuwa ameshaieleza tume kuwa fedha hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya safari ya kumpeleka mke wake India kutibiwa.
Swali jingine aliloulizwa ni kwanini hakufuata sera za matibabu zinazomhusu mtumishi wa umma kumpeleka mgonjwa nje ya nchi kupata matibabu na kujiamulia kumwomba fedha Rugemalira.
Katika majibu yake mtuhumiwa alisema kuwa anazitambua kanuni hizo lakini aliona kulikuwa na  muda mfupi wa kupeleka maombi na kama angefuata taratibu hizo angechelewa kwani marehemu mke wake alikuwa na hali mbaya.
Swali jingine lilihusu kama kweli aliona kutuma maombi katika Wizara ya Afya angechelewa na ni kwa nini baada ya fedha hiyo kuingia alienda kuitoa tofauti na ilivyoeleza awali kuwa ilikuwa ya kwenda kumtibia mkewe wakati marehemu mke wake katika nyaraka zilizowasilisha hiyo zinaonesha safari yake ya kwenda India ilikuwa  Agosti 2014.
Mtuhumiwa pia alitakiwa aeleze maana ya TCIA na wadau wa taasisi hiyo ambapo alijibu kuwa wadau wao ni serikali, wafanyabiashara, na hata wananchi.
Jibu hilo liliifanya tume imshangae mtuhumiwa iwapo alimchukulia Rugemalira kuwa ni mdau wao.
Swali la mwisho aliloulizwa ni  iwapo Sh. Milioni 80 alizopewa zilikuwa zawadi ama mkopo.  Mtuhumiwa alijibu fedha hiyo ilikuwa ni ‘profit loan’  ambapo alidai maana yake ni “mtu anakupatia pesa halafu unakuwa unamlipa kidogokidogo.”
Jaji Msami alimalizia kwa kusema utetezi wa mlalamikiwa ulikinzana na na maelezo yake katika nyaraka alizoziwasilisha hivyo adhabu kali itatolewa mara tume itakapomaliza kazi yake.